1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Biden alaani mauaji yanayochochewa na ubaguzi wa rangi

29 Agosti 2023

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kukomeshwa kwa mauaji yanayochochewa na chuki dhidi ya watu weusi na kusisitiza kuwa kukaa kimya kunachukuliwa kama kuunga mkono mauaji ya aina hiyo.

https://p.dw.com/p/4VgJP
Rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano na familia ya mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King
Rais wa Marekani Joe Biden katika mkutano na familia ya mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King Picha: Chris Kleponis/UPI Photo/IMAGO

Biden ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukumbu ya matembezi ya "March on Washington" yaliyoongozwa na mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King.

Soma pia: Mkutano wa UN kupinga ubaguzi wa rangi wasusiwa na baadhi ya mataifa 

Katika hotuba ya kihistoria ya "Nina Ndoto," mwanaharakati huyo aliihimiza serikali ya Marekani kuhakikisha haki sawa kwa watu weusi.

Wito wa Biden ameutoa baada ya mwanamume mzungu mwenye umri wa miaka 21 kuwashambulia kwa risasi na kuwauwa watu watatu weusi kwenye duka moja liitwalo Dollar General mwishoni mwa juma.

Mkuu wa polisi wa Jacksonville alisema kuwa shambulio hilo lililochochewa na chuki dhidi ya watu weusi.

Biden amesema katika mkutano uliofanyika katika Ikulu na kuhudhuriwa na watetezi wa haki za binadamu na watoto wa Marthin Luther King Jr. kwamba "hawapaswi kuruhusu chuki itawale, na kwamba visa hivyo vinaongezeka."

Ametoa wito wa kukomeshwa kwa "vurugu zinazochochewa na chuki" ambazo mamlaka zinasema zilimchochea mwanamume mzungu kuwashambulia kwa risasi watu watatu weusi kwenye duka la Dollar General jimbo la Florida.

Kamala Harris: Kuna mengi yanayotuunganisha

Familia ya mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King katika maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukumbu ya matembezi ya "March on Washington" katika ikulu ya White House.
Familia ya mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King katika maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukumbu ya matembezi ya "March on Washington" katika ikulu ya White House.Picha: Chris Kleponis/UPI Photo/IMAGO

Mshambuliaji huyo, mwanamume mzungu mwenye umri wa miaka 21, alivaa barakoa na kuwafyatulia risasi watu weusi katika duka la Dollar General katika kile mamlaka imeeleza kuwa ni uhalifu uliochochewa na chuki.

Polisi imesema mshambuliaji huyo, ambaye pia alikuwa amechapisha kauli za kibaguzi, baadaye alijiua.

Biden amesema wanaweza kukomesha mauaji kama hayo kwa "kuzungumza moja kwa moja na Wamarekani kwa sababu wengi wanakubaliana na mitazamo inayojadiliwa hapa," akiashiria wanaharakati wa kutetea haki za binadamu waliohudhuria mkutano katika ikulu ya White House.

Soma pia: Maelfu waandamana Ujerumani kupinga ubaguzi

Makamu wa rais Kamala Harris, Mmarekani wa kwanza mweusi kuchaguliwa katika nafasi hiyo, pia alikuwemo kwenye mkutano huo na kusema kwamba, Wamarekani wana mengi zaidi ya kuwaunganisha tofauti na yanayowatenganisha.

"Hata hivyo kuna watu ambao wanajaribu kwa makusudi kututenganisha sisi kama taifa na ninaamini kila mmoja wetu ana jukumu, jukumu la kutoruhusu makundi kama hayo kuvuruga umoja wetu," alisema.