1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hukumu ya kifo cha Floyd yangojewa kwa hamu Minneapolis

Sylvia Mwehozi
20 Aprili 2021

Jopo la majaji limekutana siku ya pili ya kesi ya afisa wa zamani wa polisi wa Minneapolis Derek Chauvin ambaye anakabiliwa na mashitaka ya mauaji baada ya kumkandamiza kwa goti Mmarekani mweusi George Floyd

https://p.dw.com/p/3sHp4
USA I George Floyd Memorial in Minneapolis
Picha: Mark Hertzberg/ZUMA Wire/picture-alliance

Jopo hilo la majaji 12 lilitarajiwa kuzingatia wiki tatu za kusikiliza hoja za mashahidi 45, wakiwemo wapita njia na wataalamu wa matibabu, pamoja na kutizama ushahidi wa video kwa masaa kadhaa. Chauvin ambaye ni afisa mzungu amekana shitaka la mauaji ya kukusudia, na mauaji ya kutokusudia.

Baada ya kusikiliza hoja za kufunga kwa muda mrefu hapo Jumatatu jopo hilo litalazimika kufikia uamuzi wa pamoja juu ya kila shtaka ili kumtia hatiani au kumwachia huru. 

Katika hoja hizo waendesha mashitaka walilieleza jopo la majaji kwamba afisa huyo alitakiwa "kujua" kwamba alikuwa akikandamiza uhai wa Floyd mara baada ya kulia mara nyingi kwamba anashindwa kupumua na baadae kukaa kimya.

Kesi hiyo inategemea ikiwa jopo la majaji  linaamini hoja za upande wa mashtaka

kwamba Chauvin alitumia nguvu kupindukia, na kwa hivyo ilikuwa ni haramu, na nguvu hizo ndizo zilizochangia kumuua Floyd.

Minneapolis George Floyd Proteste
Maandamano mjini Minneapolis Picha: Octavio Jones/REUTERS

Upande wa utetezi umepinga kwa hoja kwamba Chauvin alitekeleza majukumu yake kama "afisa yeyote wa polisi" ambavyo angetakiwa kufanya na wakajaribu kuibua mashaka juu ya sababu iliyochangia kifo cha Floyd, wakisema ni matatizo ya ugonjwa wa moyo au hata moshi kutoka gari la polisi la karibu unaweza kuwa sababu.

Chauvin alimkandamiza Floyd na goti kwa zaidi ya dakika tisa nje ya duka ambalo mwanaume huyo alidaiwa kuwa alinunua sigara kwa fedha bandia.

Wakati huohuo utawala Biden unapima jinsi ya kushughulikia uamuzi utakaotolewa katika kesi dhidi ya Chauvin, pamoja na kuzingatia ikiwa Rais Joe Biden atalihutubia taifa na kupeleka vikosi vyenye mafunzo maalum.

Ikulu ya Marekani White House imekuwa ikifuatilia kwa ukaribu kesi inayoendelea Minneapolis na kisha ufyatuaji rasasi mwingine uliofanywa dhidi ya Mmarekani mweusi wiki iliyopita na afisa wa polisi wa kizungu, na inajiandaa kwa uwezekano wa machafuko ikiwa uamuzi wa hatia hautofikiwa katika kesi hiyo. 

Maafisa wa ikulu wamesema Biden anaweza pia kuzungumza baada ya hukumu kutolewa.

Hukumu hiyo na matokeo yake vitakuwa mtihani kwa Biden, ambaye ameahidi kusaidia kupambana na ubaguzi wa rangi ndani ya  polisi, kuzisaidia jamii za wamarekani weusi ambao walimuunga mkono kwa idadi kubwa mwaka jana katikati mwa maandamano ya nchi nzima baada ya kifo cha Floyd na kuanzisha tena mjadala wa kitaifa juu ya masuala ya ubaguzi wa rangi.