1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Polisi: Kifo cha Mmarekani mweusi Minneapolis, bahati mbaya

13 Aprili 2021

Mkuu wa polisi huko Minneapolis, amesema polisi aliyemuua kwa kumpiga risasi Mmarekani mweusi mjini humo hakunuia kumuua kwa kuwa alitoa bastola yake kwa bahati mbaya wakati mtu huyo alipokuwa akipambana na polisi.

https://p.dw.com/p/3ruRa
USA Minneapolis Proteste nachdem die Polizei einen Schwarzen erschossen hat
Picha: Spencer Platt/Getty Images

Haya yanakuja wakati ambapo maafisa wa polisi mjini humo wamepambana na waandamanaji kwa usiku wa pili mfululizo.

Mkuu wa polisi wa Kituo cha Brooklyn Tim Gannon ameelezea mauaji ya Daunte Wright mwenye umri wa miaka 20 kama tukio lililofanyika kibahati mbaya.

Kulikuwa na waranti wa kumkamata Daunte Wright

"Ninapoutazama ukanda wa video na kusikiliza amri ya afisa wa polisi, nina imani kwamba afisa huyo alikuwa na nia ya kutumia bastola ya shoti ila badala yake akampiga risasi moja ya moto bwana Wright. Kutokana na jinsi nilivyowaona maafisa walivyoshtuka mara baada ya tukio hilo, kivyangu naona hii ilikuwa ajali ambayo ilisababisha kifo cha bwana Wright," alisema Gannon.

USA Minneapolis Proteste nachdem die Polizei einen Schwarzen erschossen hat
Mkuu wa polisi wa kituo cha Brooklyn Tim GannonPicha: Stephen Maturen/Getty Images

Wright alikuwa ametolewa nje ya gari lake na maafisa wa polisi waliokuwa wanajaribu kumfunga pingu baada ya kuona kwamba muda wa kulisajili gari lake ulikuwa umepita na kwamba kulikuwa na waranti wa kumkamata. Ila alianza kupambana nao na hatimaye akafanikiwa kujitoa mikononi mwao na akarudi ndani ya gari lake.

Alipokuwa akijaribu kufunga mlango ili atoroke, afisa wa polisi ambaye ametajwa kama Kim Potter alisikika mara kadhaa katika kamera wanazovaa polisi kwenye nguo zao Marekani, akimwambia kwamba atatumia bastola ya shoti ya umeme lakini badala yake alimfyatulia risasi kwa karibu wakati gari hilo lilipokuwa linaondoka kwa kasi. Baada ya hapo afisa huyo wa kike alisikika akilaani kumpiga risasi ya moto.

Na sasa wakionekana kupuuza amri ya kutotoka nje usiku iliyotangazwa na gavana wa jimbo hilo Tim Walz kufuatia usiku mzima wa maandamano, watu kadhaa waliondoka kutoka kwenye maombolezo ya kifo cha Wright na kujiunga na mamia ya waandamanaji waliokusanyika nje ya kituo cha polisi cha Brooklyn. Baadhi ya waandamanaji waliwakabili polisi ambao walitumia mabomu ya kutoa machozi na risasi za mpira kuwatawanya waandamanaji hao.

Kuna hasira na uchungu mwingi miongoni mwa Wamarekani weusi

Rais Joe Biden amelizungumzia tukio hilo na alikuwa na haya ya kusema.

Kifo cha Mmarekani mweusi chachoea maandamano

"Tunajua hasira na uchungu ulio katika jamii ya Wamarekani weusi ni kweli, si jambo la utani na lina matokeo yake ila hilo si sababu ya machafuko au uporaji. Na kwa hiyo swali ni, jinsi tunavyohakikisha kwamba suala hili linafanyiwa uchunguzi wa kina kubaini ukweli. Hadi hilo lifanyike, ninatoa wito wa amani na utulivu," alisema Biden.

Tukio hilo la kuuwawa kwa Wright na matokeo yake limelikumba eneo ambalo tayari liko kwenye mzozo. Kijana huyo ameuliwa maili kumi tu kutoka mahakama inayosikiliza kesi ya afisa wa zamani wa polisi wa Minneapolis Derek Chauvin anayekabiliwa na mashtaka ya kumuua mtu mwengine mweusi George Floyd mwezi Mei mwaka jana.