1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mkutano wa UN kupinga ubaguzi wa rangi wasusiwa na baadhi

Sudi Mnette
23 Septemba 2021

Mkutano wa Umoja wa Mataifa wa kupinga ubaguzi wa rangi umesusiwa na baadhi ya mataifa yakiwemo Israel na Marekani.

https://p.dw.com/p/40gOl
USA New York | UN-Jahresversammlung | Félix Tshisekedi
Picha: Giscard Kusema

Mkutano wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa jana Jumatano umetoa ahadi ya kuongeza maradufu jitihada ya kukabiliana na vitendo vya ubaguzi wa rangi duniani kwa zingatio la maazimio ya kongamano ya kupinga ubaguzi rangi la 2001 la Afrika Kusini.

Kwa kuufanyia marejeo mkutano huo wa Durban, Afrika Kusini uliofanyika takribani miongo miwili iliyopita, kulipitishwa azimio ambalo lilionesha kiwango fulani cha kupigwa hatua katika vita dhidi ya ubaguzi wa rangi, ingawa bado kunatajwa ongezeko la vitendo hivyo na kutokuwepo kwa hali ya kuvumiliana kunakowakabili watu wenye asili ya Afrika na makundi mengine.

Hayo pamoja na mambo mengine kumetolewa mfano katika katika kambi za wakimbizi, kwa makundi tofauti ya watu wakiwemo vijana, wazee, wenye ulemavu hadi wasio na makazi.

Masuala ya fidi na haki kwa wenye kubaguliwa yamepigiwa chapuo.

USA New York | UN-Jahresversammlung | Félix Tshisekedi
Rais Tshisekedi akihutubia Hadhara KuuPicha: Giscard Kusema

Katika mkutano huu wa sasa wa Baraza Kuu ya Umoja wa Mataifa pamoja na mengineyo kumezingatiwa masuala ya fidia na haki wenye kubaguliwa, zingatio likiwa athari za utumwa, ukoloni na mauwaji ya halaiki, na kuwataka watu wenye asili ya Afrika kutafuta stahili zao kwa kutumia taasisi za kimataifa.

Akichangia kwa njia ya video, Rais wa Afrika Kusini, Cyril Ramaphosa amesema mamilioni ya wenye asili ya Afrika ambao waliuzwa utumwani wamesalia katika mkwamo, wanaishi pasipo maendeleo, kukosa fursa, kubaguliwa na umasikini. Kutokana na hayo kiongozi huyo wa Afrika Kusini amelitaka Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa kuchukua hatua dhidi yale maovu yalitokea katika kipindi hicho alichokiita kama nyakati za giza.

Rais Tshisekedi wa DRC amesema fidia itatibu majeraha kwa waathirika.

Rais wa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, Felix Tshisekedi kadhalika amesema ulipaji wa fidia si kwamba utabainisha makosa yaliofanyika wakati huo lakini pia kutibu majeraha ubaguzi na ukandamizaji, vilivyojengwa katika misingi ya utumwa, ubaguzi  wa rangi na ukoloni.

Azimio la baraza hilo pia lilizingatia maovu yanayosababishwa na chuki za kidini ikiwemo wale wanauupinga Uislamu, chuki dhidi ya wageni na upendeleo dhidi ya Wakristo.

Lakini Israel, Marekani na mataifa mengine yaliususisa mkutano huo kwa sababu uliendelea na ajenda ya malalamiko ya mkutano wa Durban wa miaka 20 iliyopita. Inatajwa Marekani na Israel walijiondoa kwa sababu kuliandaliwa tamko ambalo lilikuwa likilaani vitendo vya Israel dhidi ya Wapalestina.

Jamaica, ambayo ilishiriki katika mkutano huo wa Jumatano ilisema hakukuwa na miito ya kutosha ya kulipa fidia iliyotokana na madhira ya utumwa katika ulimwengu wa siasa za sasa.

Mkutano huo, unaokwenda samba na mkutano wa kila mwaka wa Baraza Kuu la Umoja wa Mataifa viongozi wa ulimwengu walisema ubaguzi wa rangi uliwekwa wazi zaidi katika kipindi cha janga la virusi vya corona, na kitendo cha mauwaji ya 2020 ya Mmarekani mweusi, George Floyd, kumezidisha harakati za kupinga vitendo hivyo katika kila pembe ya ulimwengu.

Chanzo: AP