1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Xi asema msaada wa China kwa Afrika hauna tambo

Josephat Charo
3 Septemba 2018

Rais wa China Xi Jinping amewaambia marais wenzake kutoka barani Afrika pamoja na viongozi wa kibiashara kwamba uwekezaji wa China katika bara hilo hauna mafungamano yoyote ya kisiasa.

https://p.dw.com/p/34Chl
China Xi Jinping
Picha: picture-alliance/AP Photo/N. H. Guan

Xi ameyasema hayo leo wakati wa ufunguzi wa mkutano wa siku mbili kati ya China na Afrika mjini Beijing utakaotuwama juu ya mradi wake wa kimataifa wa ujenzi wa miundombinu ya usafiri na barabara - Belt and Road Initiative. Mradi huo unalenga kuboresha uwezo wa China kuyafikia masoko ya kimataifa na raslimali, na kuimarisha ushawishi wa utawala wa Beijing katika mataifa ya nje.

Rais huyo wa China ametangaza kutoa dola bilioni 60 kwa njia ya misaada, uwekezaji na ufadhili barani Afrika. Aliyasema hayo mbele ya mkutano huo unaohudhuriwa na zaidi ya wakuu 30 wa nchi na serikali kutoka barani Afrika, pamoja na mamia ya wajumbe wa kibiashara. Katika mkutano wa mwisho kati ya China na Afrika uliofanyika mjini Johannesburg nchini Afrika Kusini mwaka 2015, Xi aliahidi mikopo na uwekezaji wa thamani ya dola bilioni 60 barani Afrika katika kipindi cha miaka mitatu.

Tayari miradi mikubwa mikubwa ya China imeanza kuibadili taswira ya Afrika. Nchini Kenya, Nigeria, Ethiopia, Tanzania, Angola na Morocco, Wachina wamejenga njia muhimu za reli, maelfu kadhaa ya kilomita za barabara, hospitali na majengo ya serikali. Wawekezaji kutoka China hata hugharamia miji mizima, kama vile mji wa Nova Cidade de Kilamba nchini Angola wenye ukubwa wa karibu kilomita 9 za mraba.

Ruanda Besuch Präsident Xi Jinping China
Rais Xi, kulia, akiwa na rais Paul Kagame wa Rwanda, alipozuru Kigali Julai 23, 2018Picha: Getty Images/AFP/S. Maina

"Viongozi wengi wa Afrika wanakaribisha jinsi China inavyojishughulisha Afrika kama mbadala wa kile wanachokiona kuwa ni mienendo ya shingo upande ya Marekani na bara la Ulaya," alisema Sabine Mokry, mtafiti katika taasisi ya China ya Merics mjini Berlin.

Nchi zinazopokea msaada wa China zakabiliwa na madeni makubwa

China imetoa mikopo ya mabilioni ya fedha kwa nchi za Asia na Afrika kwa ajili ya ujenzi wa barabara, reli, bandari na miradi mikubwa ya miundombinu. Lakini wakosoaji wanaonya kwamba mradi huo kipenzi cha rais Xi unazizika nchi kadhaa chini ya shimo la deni kubwa.

"China haiingilii mambo ya ndani ya Afrika na wala hailazimishi ari yake kwa Afrika," alisema Xi. "Ushirikiano wa China na Afrika umelenga changamoto za maendeleo. Raslimali kwa ajili ya ushirikiano wetu hazitakiwi kutumika kwa miradi isiyokuwa na tija, lakini katika maeneo zinakohitajika zaidi," akaongeza kusema.

Hata hivyo Xi alikiri kuna haja ya kutathimini gharama za miradi na kuhakikisha maandalizi yanafanya kupunguza uwezekano wa hasara za uwekezaji na kuufanya ushirikiano kuwa endelevu.

Utafiti uliofanywa na Taasisi ya Maendeleo ya Kimataifa, inayotoa ushauri ya nchini Marekani, ulibaini kuwepo wasiwasi mkubwa kuhusu ukuaji wa deni la kigeni katika nchi nane barani Asia, Ulaya na Afrika zinazopokea fedha za mradi wa China wa ujenzi wa miundombinu.

Rais wa Rwanda, Paul Kagame, ambaye ndiye mwenyekiti wa Umoja wa Afrika, alipuuzilia mbali wasiwasi huo akisema mjadala kuhusu "mitego ya deni" ni jitihada za kuudumaza ushirikiano na maingiliano kati ya Afrika na China.

Mwandishi: Josephat Charo/dpae/afpe/reuters

Mhariri: Mohammed Khelef