1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaPakistan

Pakistan kukutana kwa dharura baada ya kushambuliana na Iran

Grace Kabogo
19 Januari 2024

Waziri Mkuu wa Pakistan, Anwar-ul-Haq Kakar, leo anafanya mkutano wa dharura wa usalama na wakuu wa jeshi na ujasusi, kuhusu msuguano kati yake na Iran.

https://p.dw.com/p/4bRgc
Waziri Mkuu wa Pakistan Anwar-ul-Haq Kakar(kushoto) akisalimia na Rais wa China, Xi Jinping
Rais wa China Xi Jinping alipokutana na Waziri Mkuu wa Pakistan Anwar-ul-Haq Kakar mjini Beijing 19.10.2023. China imejitolea kuwa mpatanishi wa mvutano baina ya Pakistan na IranPicha: Huang Jingwen/Xinhua/picture alliance

Waziri wa Habari wa Pakistan Murtaza Solangi amesema mkutano huo unafanyika baada ya nchi hizo mbili kushambuliana kwa droni na makombora.

Kwa mujibu wa Solangi, mkutano huo utajadili maslahi mapana ya usalama wa taifa baada ya mashambulizi kati ya Iran na Pakistani.

Umoja wa Mataifa na Marekani zimehimiza ustahimilivu na kujizuia, huku China ikijitolea kuwa mpatanishi katika mzozo huo.

Afisa wa usalama wa Pakistan amesema mkuu wa majeshi na mkuu wa idara za upelelezi watahudhuria mkutano huo.

Waziri Mkuu Kakar jana alikatisha ziara yake huko Davos, Uswisi alikokuwa anahudhuria mkutano wa Jukwaa la Uchumi Duniani.