1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wanaharakati wapinga sheria za kunyima dhamana Tanzania

Mohammed Khelef
4 Oktoba 2021

Mashirika ya haki za binaadamu nchini Tanzania yanasema kuna haja kufanyiwa mabadiliko sheria zinazomnyima dhamana mtuhumiwa kwa vile siyo tu zinabinya haki za msingi kwa raia, bali pia zimepitwa na wakati.

https://p.dw.com/p/41FCW
Tansania Pressekonferenz zu Übegriffen auf Journalisten
Picha: DW/S. Khamis

Kulingana na utafiti uliofanywa na Kituo cha Sheria na Haki za Binadamu (LHRC), Tanzania ni nchi pekee ambayo imeendelea kuongeza makosa yasiyokuwa na dhamana tofauti na nchi nyingine za jirani zinazoelezwa kuwa na nafuu kubwa.

Kwa mfano, watafiti wanasema idadi ya makosa yasiyokuwa na dhamana yameongezeka kutoka yale ya awali ambayo ni mauwaji na uhaini hadi kufikia mengine kama vile ya uhujumu uchumi, ugaidi pamoja na na utakatishaji wa fedha.

Akitoa ulinganifu wa hali ya makosa yasiyo na dhamana kwa Tanzania na nchi nyingine jirani, Mkurugenzi Mtendaji wa kituo cha sheria na haki za binadamu, Anna Henga amesema kuna tofauti kubwa inayoonekana.

Tafauti ya sheria Bara na Zanzibar

North Mara Gold Mine in Tansania Helen Kijo-Bisimba Direktorin LHRC
Mkurugenzi wa zamani wa LHRC, Helen Kijo-Bisimba.Picha: DW/J. Hahn

Utafiti huo umebainisha kuwa, ingawa Zanzibar ni sehemu ya Jamhuri ya Muungano wa Tanzania lakini imekuwa na sheria zake zinazohusu haki jinai. Sheria visiwani humo zimeweka ukomo maalumu kwa kesi zozote ambao uchunguzi wake bado haujakamilika. Muda huo ni miezi sita.

"Kutokana na yale yaliyoibuliwa kwenye utaifiti huo, watetezi hao wametaka kuanzishwa mchakato ambao utahakikisha sheria zote zinazobinya kutokuwepo kwa dhamana zinafanyiwa mabadiliko," anasema afisa usisimuzi wa LHRC, Raymond Kanegene.

Kuwepo kwa sheria hizo kumefanya idadi kubwa ya watuhumiwa kuendelea kusota rumande kwa muda mrefu na ingawa baadhi ya watuhumiwa kesi zao zimekuwa zikifutwa, lakini hakuna fidia yoyote inayotolewa dhidi yao.

Hivi karibuni ofisi ya mkurugenzi wa mashtaka imekuwa ikichukua mwelekeo wa kuzifuta baadhi ya kesi hizo ikieleza kutokuwa na nia ya kuendelea nazo. Baadhi yao ni wale waliokuwa mahabusu kwa miaka mingi. 

Imetayarishwa na George Njogopa, DW Dar es Salaam