1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Upinzani washinda uchaguzi wa bunge nchini Korea Kusini

Sylvia Mwehozi
11 Aprili 2024

Vyama vya upinzani vya kiliberali vya Korea Kusini vimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumatano. Waziri Mkuu wa nchi hiyo Han Duck-Soo tayari ameelezea dhamira yake ya kujiuzulu.

https://p.dw.com/p/4edrh
Uchaguzi wa bunge-Korea Kusini
Mpiga kura akishiriki uchaguzi wa bungePicha: Lee Jin-man/AP/picture alliance

Vyama vya upinzani vya kiliberali vya Korea Kusini vimepata ushindi wa kishindo katika uchaguzi wa bunge uliofanyika siku ya Jumatano. Ushindi huo ni pigo kubwa kwa Rais Yoon Suk Yeol na chama chake cha kihafidhina.

Duru zinasema kuwa Waziri Mkuu wa nchi hiyo Han Duck-Soo tayari ameelezea dhamira yake ya kujiuzulu baada ya chama chake kuangushwa na upinzani na kushindwa kupata wingi wa viti bungeni.

Takwimu kutoka Tume ya Taifa ya Uchaguzi na ripoti za vyombo vya habari zinaonyesha kwamba, chama cha Democratic Party DP kinatarajiwa kunyakua zaidi ya viti 170 kati ya 300 katika bunge jipya, baada ya zaidi ya asilimia 99 ya kura kuhesabiwa.  

Chama kingine cha kiliberali kinachozingatiwa kuwa mshirika wa DP kinatarajiwa kushinda angalau viti 10. 

Uchaguzi huo wa bunge uliokuwa na ushindani mkali ulichukuliwa kama kipimo kwa Rais Yoon, ambaye umaarufu wake umegubikwa na mgogoro wa kupanda kwa gharama ya maisha na kashfa nyingi za kisiasa.