1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN yaitaka Urusi ikiri kukishambulia kijiji Ukraine

Bruce Amani
31 Oktoba 2023

Wapelelezi wa Umoja wa Mataifa wameihimiza Urusi kukiri kuhusika na shambulizi la kombora kwenye kijiji kimoja cha Ukraine lililowauwa raia 59.

https://p.dw.com/p/4YFC3
Mwanajeshi wa Ukraine akijaribu kuteguwa bomu la ardhini.
Mwanajeshi wa Ukraine akijaribu kuteguwa bomu la ardhini.Picha: Sofiia Gatilova/REUTERS

Wameitaka Urusi ifanye uchunguzi wa wazi kuhusu kilichotokea, itoe fidia kwa waathiriwa na iwawajibishe waliohusika.

Ujumbe wa Umoja wa Mataifa wa Ufuatiliaji wa Haki za Binaadamu nchini Ukraine umesema katika ripoti iliyochapishwa leo kuwa ina ushahidi wa kutosha kuamini kuwa kombora la Urusi la masafa mafupi huenda lilisababisha mlipuko huo katika kijiji cha Hroza mnamo Oktoba 5.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya watofautina kuhusu msaada Ukraine

Shambulizi hilo lililopiga mgahawa mmoja kijiji hapo lilikuwa moja ya mashambulizi makali zaidi kuwahi kufanywa tangu vikosi vya Urusi vilianzisha uvamizi kamili nchini Ukraine miezi 20 iliyopita.

Familia zote ziliangamia wakati zikiwa katika hafla ya kumuaga askari wa eneo hilo aliyeuawa wakati akipigana na askari wa Urusi.

Mripuko huo uliwauwa wanawake 36, wanaume 22 na mvulana wa umri wa miaka minane.