1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

UN lina wasiwasi juu ya masharti ya Syria kuruhusu misaada

15 Julai 2023

Umoja wa Mataifa umeonyesha wasiwasi juu ya barua kutoka serikali ya Syria iliyotoa ruhusa ya kutumika kwa njia ya Bab al-Hawa kusafirisha misaada ya kibinadamu kuelekea kaskazini magharibi mwa Syria ikitokea Uturuki.

https://p.dw.com/p/4TwR1
Wafanyakazi wa misaada ya kiutu katika ghala karibu na Bab al-Hawa
Wafanyakazi wa misaada ya kiutu katika ghala karibu na Bab al-HawaPicha: Omar Haj Kadour/AFP/Getty Images

Hii ni baada ya idhini ya baraza la usalama la Umoja wa Mataifa la kutumia njia hiyo kukamilika siku ya Jumatatu.

Katika barua kwa baraza la usalama iliyoandikwa na serikali na iliyoonekana na shirika la habari la Reuters, ofisi ya Umoja wa Mataifa ya uratibu wa misaada ya dharura OCHA, imeonyesha mashaka juu ya masuala mawili iliyoyaita "yasiokubalika."

Soma zaidi: Syria: Zaidi ya muongo mmoja wa mateso na mauaji

OCHA imeeleza kuwa, ruhusa kutoka kwa serikali ya  Syria inaweza kutafsiriwa kuwa msingi wa Umoja wa Mataifa kuendelea na oparesheni zake za kusafirisha misaada ya kibinadamu kupitia kivuko cha Bab al-Hawa kwa muda uliowekwa.

Syria imetoa ruhusa kwa Umoja wa Mataifa kutumia njia ya Bab al-Hawa kwa miezi mingine sita  lakini kwa masharti kadhaa. Moja ya masharti hayo ni Umoja wa Mataifa kutowasiliana kwa namna yoyote na mashirika au makundi yanayochukuliwa na serikali ya Syria kama ya kigaidi.