1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ulimwengu waadhimisha siku ya sayari ya dunia

Halima Gongo22 Aprili 2024

Wakati hivi leo ulimwengu ukiadhimisha siku ya Sayari ya Dunia, Jimi Cohen, raia wa Australia na mwanzilishi mwenza wa shirika la Treegens DAO, ameweka rekodi ya kupanda miti mingi zaidi kwa kipindi cha masaa 24.

https://p.dw.com/p/4f3xo
Uhispania-Barcelona
Sehemu ya ardhi huko BarcelonaPicha: Emilio Morenatti/AP Photo/picture alliance

Cohen amefanikiwa kuipanda mikoko elfu 30,279 katika eneo la Majoreni, Kaunti ya Kwale, iliyoko Pwani ya Kenya akivunja rekodi iliyokuwa imewekwa na Antoinne Moses, raia wa Canada aliyepanda miti elfu 23,060 mwaka 2021.

Tangu jana, mwendo wa saa sita mchana, raia huyu wa Australia alianza upandaji wa miche ya mikoko katika eneo la Majoreni, Kaunti ya Kwale, hapa Pwani ya Kenya. Shughuli hiyo imekamilika leo Jumatatu, wakati ulimwengu ukiadhimisha siku ya Sayari ya Dunia.

Cohen anasema azma hii imechangiwa na jitihada za kutumia miti kusafisha mazingira  na kuishawishi dunia kuchukua hatua ya kuyalinda mazingira. Kulingana naye, alilichagua bara la Afrika na hasa Pwani ya Kenya kwa sababu ya usalama na pia kuvutiwa na watu wa Majoreni, ambao wamekuwa wakipanda mikoko kuyalinda mazingira.  “Ni nchi ya kuvutia na ina mandari ya kupendeza na wenyeji pia wanayajali mazingira na ni kuzuri kwa kupanda mikoko, nchini australia kupanda mikoko kuna changamoto kwa sababu kuna mamba wengi kwa hiyo si salama ndio maana nilichagua Kenya, hata watu wanaelewa kuhusu mazingira. Hii ni Mara yangu ya tatu kujaribu kuvunja rekodi, ikotokea sijafaulu basi haitakuwa mwisho wangu nitajaribu Tena.”

Ardhi kavu huko Vietnam
Sehemu ya ardhi iliyomegeka huko VietnamPicha: Nhac Nguyen/AFP

Soma: Je, ni nini maana ya upotoshaji kuhusu tabia nchi?

Hii ni mara yake ya tatu kujaribu kuvunja rekodi hii ya upandaji wa miche. Anasema amekuwa akifanya mazoezi kwa takribani mwaka mmoja. Kabla ya kutunukiwa taji hilo, shughuli nzima itaratibiwa na shirika la Guiness World Record. Iwapo atashinda, Cohen atakuwa binadamu wa kwanza duniani kupanda miche zaidi ya elfu thelathini ya mikoko kwa masaa 24 mfululizo.

Livingstone Kitawi, afisa wa Idara ya kuhifadhi misitu nchini Kenya pamoja na wenzake waliongoza shughuli ya kunakili idadi ya miche pamoja na kumlinda. “tumeweza kusaidia katika kuhesabu, kipindi cha kwanza tulikuwa tunafanya masaa manne manne,halafu napumzika napisha wenzangu, tulikuwa zaidi ya watu nane hapo tukibadilishana kwa hayo masaa ishirini na nne,tumeweza kutembea na wao na pia tukajua uwezo wetu kuwa tunaweza kufanya kazi masaa ishirini na nne bila kupumzika na pia bila kuchoka .“

Wanakijiji wa Majoreni wameiambia kuwa wafurahishwa kwa kijiji chao kuchaguliwa kwa kampeni hii. Mmoja wao, Omari Bakari, anasema miche iliyopandwa imewapunguzia kazi kubwa wanamazingira. Bakari ameahidi kufuatilia miche hiyo kuhakikisha imechipua. siku ya Leo tukona furaha, mwanzo sisi ndio huwa walindaji bora wa mazingira, kuna Kama vikundi vinne vya wapanzi wa miti katika sehemu yetu Hii ya majoreni.”

Soma pia: Joto la 2023 halikuwahi kushuhudia miaka 100,000 iliyopita

Kaulimbiu ya maadhimisho ya mwaka huu wa 2024 kwa Siku ya Sayari ulimwenguni ni "Sayari Dhidi ya Plastiki", ikitowa ujumbe wa kuongeza ufahamu wa watu kuhusu hatari za kiafya za plastiki, kwa lengo la kukomesha matumizi ya plastiki. Siku hii ilianza kuadhimishwa mwaka 1970 nchini Marekani.