1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yawakamata raia watatu kwa kuifanyia China ujasusi

Sylvia Mwehozi
22 Aprili 2024

Waendesha mashitaka wa Ujerumani wamewakamata watu watatu raia wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa ajili ya idara ya usalama ya China.

https://p.dw.com/p/4f3ll
Polisi wa Ujerumani
Polisi wa UjerumaniPicha: Gianni Gattus/dpa/picture alliance

Waendesha mashitaka wa Ujerumani wamewakamata watu watatu raia wa Ujerumani kwa tuhuma za kufanya ujasusi kwa ajili ya idara ya usalama ya China.

Kwa mujibu wa ofisi ya mwendesha mashitaka ya shirikisho ya Ujerumani, watuhumiwa hao, wanaume wawili na mwanamke mmoja walikamatwa kwenye miji ya magharibi ya Dusseldorf na Bad Homburg siku ya Jumatatu.

Fuatilia habari hii:Ujerumani, China zafanya mazungumzo ya ngazi ya juu 

Wanashukiwa kuwa walikuwa wakifanya kazi na idara ya usalama ya China tangu Juni mwaka 2022 na wamekiuka sheria ya biashara ya kimataifa na malipo katika muktadha huo.

Olaf Scholz alipokuwa ziarani China
Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz na Rais wa China Xi JinpingPicha: Xie Huanchi/AP/picture alliance

Kesi hiyo inahusu utoaji wa taarifa za teknolojia ya kijeshi kwa idara ya usalama ya China. Wakati wa kukamatwa kwao, washukiwa hao walikuwa kwenye mazungumzo kuhusu miradi ya utafiti ambayo inaweza kuwa na manufaa kwa upanuzi wa nguvu za kijeshi za baharini za China, kulingana na waendesha mashtaka.

Soma: Ujerumani yazindua mkakati mpya wa kuamiliana na China

Mmoja wa washukiwa hao anasemekana kuuza taarifa za teknolojia ya ubunifu wa kijeshi kwa mfanyakazi wa idara ya usalama ya China MSS.

Washukiwa hao watafikishwa mbele ya hakimu wa Mahakama ya Shirikisho siku ya Jumatatu na Jumanne.