1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ujerumani yasubiri uamuzi wa Rais Obama juu ya Afghanistan

Kabogo Grace Patricia20 Novemba 2009

Hayo yameelezwa na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodore zu Guttenberg mjini Washington.

https://p.dw.com/p/Kbf8
Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodor zu Guttenberg, akiwa na Rais Hamid Karzai wa Afghanistan, mjini Kabul.Picha: AP

Ujerumani ambayo ni nchi ya tatu yenye wanajeshi wengi katika majeshi yanayoongozwa na Jumuiya ya Kujihami-NATO, nchini Afghanistan imesema uamuzi wake wa kupeleka majeshi zaidi nchini humo utategemea mikakati mipya ya kivita ya Rais Barack Obama wa Marekani, inayotarajiwa kutangazwa katika wiki zijazo. Kauli hiyo imetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Ujerumani, Karl-Theodore zu Guttenberg alipomtembelea Waziri mwenzake wa Marekani, Robert Gates, katika ofisi yake mjini Washington. Zu Guttenberg aliwaambia waandishi habari na kumhakikishia Gates kuwa Ujerumani itafanya uamuzi wake wenyewe na kusubiri uamuzi wa Rais Obama endapo ataongeza wanajeshi zaidi nchini Afghanistan ama la. ''Kuna mengi yaliyodhihirika kutokana na hotuba ya rais wa Marekani na kwa kuwa uhusiano ni wa kuaminiana sisi hatutozungumzia juu ya kile ambacho rais wa Marekani atakiamua siku zijazo,'' alisema zu Guttenberg.

Aidha, Waziri huyo wa Ulinzi wa Ujerumani amesema uamuzi wa nchi yake utategemea pia utendaji wa serikali ya Rais Hamid Karzai aliyeapishwa jana kwa awamu ya pili ya miaka mitano na kuahidi kukabiliana na tatizo la rushwa na kudhibiti usalama wa nchi hiyo. Aidha, Zu Guttenberg alisema jana ilikuwa siku nzuri kwa Afghanistan na sasa wanasubiri matokeo ya yale yaliyozungumzwa na Rais Karzai katika hotuba yake aliyoitoa jana baada ya kuapishwa. Amesema wanahitaji kuona vitendo zaidi kuliko maneno kutoka katika serikali ya Afghanistan. Alisema nchi wanachama wa NATO wanatarajia kuona mageuzi yatakayofanywa na Rais Karzai baada ya kuahidi kupambana na rushwa.

Pongezi za Marekani kwa EU

Kwa upande wake Waziri Gates alisema anapongeza hatua ya Umoja wa Ulaya kudhamini mkutano kuhusu Afghanistan uliopangwa kufanyika Januari, mwaka ujao. Bwana Gates alisema Marekani inatarajia kupata msaada mkubwa kuhusu Afghanistan. Waziri huyo wa Ulinzi wa Marekani alisema, ''Tutatumia msaada wote tutakaopata lakini kiukweli nafikiri katika hatua tuliyoifikia hadi sasa ni hadi rais atakapotangaza uamuzi wake. Ni mapema mno kwa taifa lolote lile kuzungumzia juu ya kuongeza wanajeshi zaidi.''

Idadi ya vikosi vya NATO huko Afghanistan

Wiki hii, Ujerumani ilitangaza kuongeza muda kwa wanajeshi wake kuendelea kuwepo nchini Afghanistan kwa mmoja zaidi licha ya wananchi wa Ujerumani kupinga uwepo wa majeshi hayo nchini Afghanistan na wasi wasi uliopo juu ya utendaji kazi katika serikali ya nchi hiyo. Kwa sasa Ujerumani ina wanajeshi 4,500 nchini Afghanistan ambao wamepiga kambi katika eneo la Kundus. Katika wanajeshi 100,000 waliopo wa NATO, Marekani ina wanajeshi kiasi 68,000. Aidha, wiki iliyopita Ujerumani ilitangaza kupeleka wanajeshi zaidi 120 huko Kundus kati ya Januari mwaka ujao.

Mwandishi: Grace Patricia Kabogo (RTRE/AFPE/APE)

Mhariri:Abdul-Rahman