1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Togo wachaguwa wabunge baada ya mageuzi tata ya katiba

Tatu Karema
30 Aprili 2024

Raia wa Togo wamepiga kura kuwachagua wabunge baada ya mageuzi tata ya katiba ambayo wapinzani wanasema yanampa Rais Faure Gnassingbe mwanya wa kuongeza muda wa kuendelea kushikilia madaraka.

https://p.dw.com/p/4fLNL
Rais Faure Gnassingbe wa Togo.
Rais Faure Gnassingbe wa Togo.Picha: Ute Grabowsky/photothek/IMAGO

Shirika la habari la AFP limeripoti kuwa vituo vya kura vilifungwa mwendo wa saa 12:00 jioni ya Jumatatu (Aprili 29) na baada ya hapo kura zikaanza kuhesabiwa.

Taarifa ya tume ya uchaguzi nchini humo ilisema kuwa huenda matokeo ya awali yangelianza kutolewa jioni hiyo hiyo.

Soma zaidi: Togo yapiga kura ya wabunge baada ya mageuzi ya kikatiba

Uchaguzi huo ulikuwa wa kuwachagua wabunge 113 na pia kwa mara ya kwanza, makamu wakuu wa mikoa 179 katika wilaya tano, ambao pamoja na madiwani watachagua baraza jipya la seneti.

Kulingana na chama tawala cha Gnassingbe, UNIR, hatua hiyo inaifanya Togo kuwa na uwakilishi zaidi, lakini vyama vya upinzani viliwahamasisha wafuasi kupiga kura dhidi ya kile walichokitaja kuwa mapinduzi ya kitaasisi.