1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Tiger Woods atoka hospitalini

Lilian Mtono
17 Machi 2021

Bingwa wa gofu ulimwenguni Tiger Woods amerejea nyumbani kwake Florida kuendelea kupata mapumziko na kupona majeraha aliyoyapata kwenye ajali mbaya ya gari.

https://p.dw.com/p/3qkcs
Genesis Invitational Golf I Tiger Woods
Picha: Ryan Kang/AP/picture alliance

Bingwa wa gofu ulimwenguni Tiger Woods amerejea nyumbani kwake Florida kuendelea kupata mapumziko na kupona majeraha aliyoyapata kwenye ajali mbaya ya gari aliyoipata katika eneo la makazi katika mji wa Los Angeles mwezi uliopita. Majeraha ya Woods yanaongeza wasiwasi kwa nguli huyo kurejea viwanjani katika siku za karibuni ama huko siku za usoni.

Woods aliandika kwenye ukurasa wake wa twitter jana Jumanne "Nina furaha kurudi nyumbani na kuendelea kupona." "Ninashukuru sana kwa msaada mkubwa na salamu nyingi za kunitia moyo ambazo nilizipata wiki zilizopita."

Woods aliumia Februari 23, siku mbili baada ya mashindano ya gofu ya Genesis Invitational yaliyofanyika kwenye uwanja wa gofu wa Riviera. Alikuwa akienda kwenye tukio la kupiga picha kwa ajili ya chaneli ya GolfTV majira ya saa moja asubuhi, wakati gari yake aina ya SUV ilipopata ajali na kupinduka.

Woods alifanyiwa upasuaji wa mifupa kwenye mguu wake wa kulia uliochukua muda mrefu katika hospitali ya Harbor-UCLA, na kwenye majeraha mengine aliyoyapata. Baadaye alihamishiwa kwenye hospitali ya Cedars-Sinai kwa ajili ya matibabu zaidi. Woods amewashukuru madaktari na watumishi wengine wa hospitali hizo kwa huduma walizompa.

Mashirika: APE