1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Ruto aitisha kikao maalum kujadili athari za mafuriko

30 Aprili 2024

Rais William Ruto wa Kenya ameitisha kikao maalum cha baraza la mawaziri kujadili hatua za kukabiliana na mafuriko ambayo yamesababisha vifo vya zaidi ya watu 170 na wengine 185,000 kuyahama makaazi yao nchini humo.

https://p.dw.com/p/4fLWm
Rais William Ruto wa Kenya.
Rais William Ruto wa Kenya.Picha: Monicah Mwangi/REUTERS

Ruto alisema kikao hicho kilitarajiwa kujadili juu ya hatua za ziada katika kushughulikia mzozo huo na kuongeza kuwa lazima serikali iwaangalie wananchi ambao ni waathirika wa mabadiliko ya hali ya hewa.

Viongozi wa vyama vya upinzani pamoja na watetezi wa haki za binadamu nchini humo wameishutumu serikali ya Ruto kwa kutokufanya ya kutosha, licha ya tahadhari iliyotolewa na mamlaka ya hali ya hewa na kuitaka itangaze mafuriko hayo kuwa janga la kitaifa.

Soma zaidi: Rais Ruto atangaza mikakati ya kukabiliana na mafuriko

Mvua kubwa kuliko kawaida ikichangiwa na hali ya El Nino imeshuhudiwa katika taifa hilo la Afrika Mashariki na kusababisha uharibifu mkubwa ikiwemo miundombinu ya barabara, kughariki kwa vijiji na kutishia uharibifu zaidi katika siku za usoni.

Katika mkasa mbaya zaidi hadi sasa, siku ya Jumatatu (Aprili 29), kingo za Bwawa la Kijabe zilipasuka na kusababisha vifo vya takribani watu 50.