1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Somalia afuta makubaliano ya Ethiopia, Somaliland

Mohammed Khelef
7 Januari 2024

Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia amesaini sheria ya kuyafuta makubaliano yaliyofikiwa na jimbo la Somaliland kuipa Ethiopia fursa ya kutumia Bahari ya Sham ili nalo litambuliwe uhuru wake na Addis Ababa.

https://p.dw.com/p/4awSf
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.
Rais Hassan Sheikh Mohamud wa Somalia.Picha: Farah Abdi Warsameh/AP/picture alliance

Akiandika kupitia mtandao wa Twitter jioni ya Jumamosi (Januari 6), Mohamud alisema makubaliano hayo yamefutwa kwa kuwa hayafai.

"Jioni hii, nilisaini sheria ya kufuta Hati ya Makubaliano kati ya serikali ya Ethiopia na Somaliland. Sheria hii ni kielelezo cha dhamira yetu ya kuulinda umoja, mamlaka na heshima ya mipaka yetu kwa mujibu wa sheria za kimataifa." Aliandika rais huyo wa Somalia.

Hata hivyo, Mohamud hakuweka bayana kile kinachosemwa na sheria hiyo mpya wala muda iliyopitishwa na bunge.

Matumaini ya nchi ya Waziri Mkuu wa Ethiopia, Abiy Ahmed, kupata fursa ya kuitumia Bahari ya Sham ni chanzo cha mzozo kwenye taifa hilo la Pembe ya Afrika na majirani zake na limezusha mashaka ya kuzuka upya kwa mapigano kwenye eneo hilo.

Ufafanuzi: Somaliland ni taifa huru?

Somalia, ambayo inaichukulia Somaliland kama sehemu ya mamlaka yake, iliyakataa makubaliano hayo yaliyotiwa saini Siku ya Mwaka Mpya, ambayo yangeliiruhusu Ethiopia - taifa lisilo mpaka wa bahari - kutumia kipande cha ardhi ya kilimota 20 kwenye bandari ya Berbera iliyo kwenye Ghuba ya Aden kwa muda wa miaka 50 kwa ajili ya jeshi lake la baharini na matumizi ya kibiashara.

Ethiopia kuutambua uhuru wa Somaliland?

Kwa upande wake, Ethiopia ingelikuwa taifa la kwanza kuitambua Somaliland kama taifa huru.

Rais  Muse Bihi Abdi wa Somaliland.
Rais Muse Bihi Abdi wa Somaliland.Picha: TIKSA NEGERI/REUTERS

Hakukuwa na taarifa ya haraka kutoka maafisa wa Somaliland wala Ethiopia juu ya hatua hiyo ya Rais Sheikh kuyafuta makubaliano yao.

Soma zaidi: Umoja wa Ulaya watia neno mkataba wa Ethiopia na Somaliland

Mnamo mwezi Oktoba, Abiy alisema "uwepo wa Ethiopia unafungamanishwa na Bahari ya Sham," akiongeza kwamba ikiwa mataifa ya Pembe ya Afrika "yanapanga kuishi pamoja kwa amani, lazima tutafute njia kugawana kwa njia ya usawa."

Mshauri wake wa masuala ya usalama amesema Ethiopia ingeliipa Somaliland hisa kwenye shirika lake la ndege, Ethiopian Airlines.