1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais wa Iran Ebrahim Raisi aanza ziara nchini Pakistan

Lilian Mtono
22 Aprili 2024

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amewasili mjini Islamabad tayari kuanza ziara ya siku tatu, huku ulinzi ukiimarishwa kwenye mji huo mkuu wa Pakistan.

https://p.dw.com/p/4f2Zn
Rais wa Iran Ebrahim Raisi
Rais wa Iran Ebrahim Raisi Picha: Vahid Salemi/AP/dpa/picture alliance

Rais wa Iran Ebrahim Raisi amewasili mjini Islamabad tayari kuanza ziara ya siku tatu, huku ulinzi ukiimarishwa kwenye mji huo mkuu wa Pakistan.

Ziara hiyo inafanyika wakati mataifa hayo mawili jirani ya Kiislamu yakisaka kurekebisha uhusiano baada ya mashambulizi ambayo hayakutarajiawa baina yao mwaka huu.

Rais Raisi anatarajiwa kukutana na Waziri Mkuu wa Pakistan Shehbaz Sharif na maafisa wengine na kutembelea jiji la Lahore mashariki mwa nchi hiyo na mji wa bandari wa Karachi, kusini mwa Pakistan.

Ziara ya Raisi ni hatua muhimu kuelekea kurekebisha uhusiano na Islamabad, ingawa kiongozi wa juu nchini Iran, Ayatollah Ali Khamenei, ndiye mwenye mamlaka ya mwisho juu ya masuala ya kitaifa kama ya sera za nyuklia.

Pakistan na Iran wamekuwa na historia ya mahusiano mabovu licha ya makubaliano kadhaa ya kibiashara, lakini kwa upande mwingine, ina mahusiano mazuri na Marekani na Saudi Arabia.