1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Ndayishimiye agusia mazungumzo na makundi ya waasi

Sylvia Mwehozi
12 Mei 2022

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema kuwa yuko tayari kwa mazungumzo na waasi wa Burundi wanaoendesha operesheni zao nchini Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo hasa upande wa mashariki.

https://p.dw.com/p/4BBWJ
Burundi Bujumbura | Evariste Ndayishimiye, Präsident
Picha: Bujumbura Amida Issa/DW

Rais Ndayishimiye ameyasema hayo katika mkutano wake wa kwanza na waandishi wa habari tangu achukue madaraka na kulitaja haswa kundi la RED-Tabara ambalo linachukuliwa na Burundi kama "magaidi" pamoja na kundi jingine la jeshi la kitaifa la ukombozi FNL.

"Kama RED-Tabara na FNL wataomba kuzungumza, tuko tayari kuwakaribisha na kuzungumza nao". Rais Ndayishimiye ameongeza kwamba "ni wajibu wa serikali kusikiliza malalamiko ya watoto wake wote na kutoa majibu," alisema Ndayishimiye akirejelea msemo wa Kirundi kwamba "nafasi ya mtoto mwenye mapungufu ni nyumbani kwao".

Kundi la RED-Tabara ambalo lilianzishwa mwaka 2011, linakadiriwa kuwa na wapiganaji kati ya 500 na 800 ambao wako mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo. Kundi hilo limetuhumiwa kufanya mkururo wa mashambulizi nchini Burundi tangu mwaka 2015.Mazungumzo kati ya Serikali ya Burundi na FNL PALIPEHUTU kufanyika hivi karibuni

Mwanasiasa wa upinzani wa Burundi anayeishi uhamishoni Alexis Sinduhije alilieleza shirika la habari la AFP mnamo mwezi Novemba kwamba kundi hilo, limejiimarisha na sasa lina uwepo wake nchini Burundi. Kwa mujibu wa duru kadhaa, Sinduhije ndiye mwasisi wa harakati hizo, madai ambayo siku zote ameyakanusha.

Kongo | Besuch des Präsidenten Burundis Evariste Ndayishimiye bei Felix Tshisekedi
Rais Evariste Ndayishimiye na mwenzake Felix TshisekediPicha: Giscard Kusema

Mnamo mwezi Septemba, kundi la RED-Tabara lilidai kuhusika na shambulio kwenye uwanja wa ndege wa kimataifa wa Bujumbura, mji wa kiuchumi wa Burundi ambako mashambulizi kadhaa yalitokea katika mwezi huohuo.

Kundi jingine la FNL, linaloongozwa na jenerali aliyejitangaza mwenyewe Aloys Nzabampema, ni tawi la mabaki ya uasi wa zamani wa Agathon Rwasa ambaye sasa ni kiongozi mkuu wa upinzani nchini Burundi. Makundi yote ya FNL na  RED-Tabara yana ngome zake huko mashariki mwa Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo, eneo lililodhoofishwa na uwepo wa makundi mengi ya ndani na nje yaliyo na silaha.

Zaidi ya askari 1,000 wa Kirundi wamekuwepo kwa miezi kadhaa katika jimbo la Kivu ya Kusini ili kuwafuatilia waasi wa Red-Tabara, kulingana na duru tofauti kutoka Congo na Burundi, lakini serikali za nchi zote mbili zimekanusha shutuma hizo. Jumuiya ya kikanda ya afrika Mashariki, mwezi uliopita ilifanya mazungumzo mjini Nairobi juu ya vurugu za makundi ya wapiganaji ambayo yameikumba Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo kwa zaidi ya miongo miwili sasa.

Baada ya mkutano huo, Ndayishimeye aliwataka wanachama wa RED-Tabara kuweka chini silaha zao akiwaelezea kuwa "wahalifu", matamshi yaliyolaaniwa na kundi hilo kama "lugha ya matusi".