1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUrusi

Putin aitisha mkutano kufuatia uvamizi wa uwanja wa ndege

30 Oktoba 2023

Rais wa Urusi Vladimir Putin ameitisha mkutano wa maafisa wakuu wa usalama Jumatatu, siku moja baada ya kundi la watu kuvamia uwanja wa ndege wa jimbo la Dagestan.

https://p.dw.com/p/4YD1h
Vladimir Putin, rais wa Urusi.
Vladimir Putin, rais wa Urusi.Picha: via REUTERS

Ni baada ya ndege kutoka mji wa Tel Aviv nchini Israel kutua.

Msemaji wa ikulu ya Kremlin Dmitry Peskov amesema mkutano huo utajadili majaribio ya nchi za Magharibi kuigawa jamii ya Urusi kutokana na matukio ya Mashariki ya Kati.

Hatua hii ya Rais Putin inajiri baada ya ikulu ya Kremlin kulalamikia "uingiliaji wa nje" kwa machafuko hayo yaliyotokea katika uwanja wa ndege wa Makhachkala.

Ripoti katika vyombo vya habari vya Urusi zinaarifu kwamba mamia ya watu waliokuwa na ghadhabu waliingia katika uwanja wa ndege na kuanza kuwatafuta raia wa Israeli baada ya ndege hiyo kutoka Tel Aviv kutua.

Afisi ya Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu kufuatia tukio hilo ilisema, inatarajia mamlaka nchini Urusi ziwalinde Waisraeli na Wayahudi popote walipo nchini humo.