1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaBurundi

Ndayishimiye: Burundi bado inao maadui licha ya utulivu

13 Mei 2024

Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye amesema hali shwari ya kiusalama inayoshuhudiwa haina maana kuwa taifa hilo la Afrika Mashariki hali maadui.

https://p.dw.com/p/4fo6T
Rais wa Burundi Evariste Ndayishimiye
Rais wa Burundi Evariste NdayishimiyePicha: Tchandrou Nitanga/AFP/Getty Images

Ameyasema hayo alipokutana na maafisa wa usalama katika mikoa ya Magharibi mwa nchi hiyo ambapo leo imeadhimisha mwaka wa 9 tangu kutokea jaribio la mapinduzi ya kijeshi mnamo mwaka 2015.

Maadhimisho hayo yanafanyika wakati watu kadhaa tayari wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na kuripuwa maguruneti mwishoni mwa wiki katikati ya jiji la Bujumbura ambapo takriban watu 40 walijeruhiwa. 

Katika mkutano wake huo na maafisa usalama katika mikoa ya Bujumbura, Cibitoke, Bubanza na jiji la Bujumbura inayounda kanda ya magharibi mwa Burundi, rais Evariste Ndayishimiye amesema wamekusudia kutathmini hali ya usalama katika kanda hiyo ili kujua kipi kifanyika.

Rais Ndayishimiye amesema hata kama ipo hali ya utulivu kiusalama haiamanishi kuwa hakuna maadui.

"Nitumie fursa hii kuwapongenza kwa kazi nzuri mnayo ifanya kila kukicha. Lakini kama Nchi iko tulivu haiamanishi kuwa hakuna adui ama anaye kusudia kufanya ubaya hawezi kuja. Maadui wapo na wamekuwa wakikamatwa na walinda usalama," amesema kiongozi huyo wa Burundi. 

Maadhimisho yafanyika baada ya mkasa wa shambulizi mjini Bujumbura

Maadhimisho haya ya miaka 9 tangu kujiri jaribio la mapinduzi ya kijeshi Mei 13 mwaka 2015 yanafanyika wakati mwishoni mwa wiki wakaazi wa jiji walikabiliwa tena na mashambulizi ya maguruneti.

Maandamano ya Umma Burundi mwaka 2015
Jaribio la mapinduzi la mwaka 2015 nchini Burundi lilichochewa na ghasia zilizozuka kufuatia azma ya rais wa wakati huo Pierre Nkurunziza kuwani muhula wa tatu madarakani. Picha: PHIL MOORE/dpa/picture alliance

Msemaji wa wizara ya mamabo ya ndani Pierre Nkurikiye alisema watu wasio punguwa 38 walijeruwa na takriban watu watano wakiwa katika hali mahututi.

Watu 6 akiwemo aliyekuwa zamani askari polisi tayari wamekamatwa kwa tuhuma za kuhusika na miripuko hiyo, na watu hao wanatuhumiwa kuwa wanashirikiana na kundi la waasi la Red Tabara linalo tajwa kupewa hifadhi katika nchi jirani ya Rwanda.

Hamza Venant Burikukiye mkuu wa shirika la kiraia la Capes Plus ameagiza shughuli za vyama vya siasa kufuatiliwa kwa karibu wakati huu nchi ikijiandaa kwa uchaguzi wa mwaka ujao 2025.

Miito ya kuwepo na umakini zaidi juu ya hali ya usalama wakati huu nchi ikijianda kwa uchaguzi wa mwakani, imetolewa pia wawakilishi wa dini zinazo patika nchini.