1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Misimamo mikali ya mrengo wa kulia yaongezeka Ujerumani

20 Juni 2023

Misimamo mikali ya mrengo wa kulia imeongezeka nchini Ujerumani, kulingana na ripoti ya kila mwaka iliyotolewa na waziri wa Mambo ya ndani wa Ujerumani Nancy Feaser na Mkuu wa idara ya Ujasusi wa ndani Thomas Haldenwang

https://p.dw.com/p/4SqZ6
AfD-Demo gegen die die Regierungspolitik in Berlin
Picha: Michael Kuenne/ZUMAPRESS.com/picture alliance

Kulingana na ripoti hiyo, idadi ya watu walioorodheshwa mnamo mwaka 2022 kuwemo katika makundi ya siasa kali za mrengo wa kulia, iliongezeka kwa karibu 14.5% hadi kufikia watu 38,800 ikilinganishwa na mwaka uliopita. Moja ya sababu za idadi hiyo kuongezeka kwa kasi, ni kwamba kwa mara ya kwanza kabisa, idara ya ujajusi imewajumuisha katika orodha hiyo, wanachama wa chama cha  siasa kali za mrengo wa kulia cha Ujerumani (AfD).

Idara ya ujasusi wa ndani ya Ujerumani ilikiliainisha chama hicho kama kinachoshukiwa kuwa na itikadi kali za mrengo wa kulia, jambo ambalo lilithibitishwa na Mahakama moja mjini Cologne. Hata hivyo, AfD imekata rufaa juu ya uamuzi huo.

Ripoti hiyo inaendelea kubaini kuwa, kwa kuzingatia utofauti unaoendelea kuwepo ndani ya chama hicho katika suala la maudhui, si wanachama wote wa AfD wanaoweza kuchukuliwa kama wafuasi wanaoshabikia mikondo yenye itikadi kali.

Soma pia: Chama cha AFD kinaweza ushtakiwa kwa siasa za chuki

Idara hiyo ya ujasusi inakadiria kuwa wanachama wapato 10,200 wa AfD pamoja na kitengo cha vijana cha (Junge Alternative), wanaweza kuainishwa kama sehemu ya harakati zenye msimamo mkali.

Mkuu wa idara ya Ujasusi wa ndani wa Ujerumani Thomas Haldenwang anasema kumekuwa na mkanganyiko na imekuwa vigumu kupambanua wazi aina ya watu au kujua mipaka ya wanaojihusisha na harakati hizo za mrengo mkali wa kulia, huku akisisitiza kuwa kitisho cha ugaidi kutoka kwa watu wenye itikadi kali za Kiislamu bado kiko juu.

Siasa za mrengo mkali wa kulia ni tishio kwa Demokrasia ya Ujerumani

Bundesinnenministerin Faeser reist nach Tunesien
Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy FaeserPicha: Bernd von Jutrczenka/dpa/picture alliance

Waziri wa Mambo ya Ndani wa Ujerumani Nancy Faeser amesema tishio kubwa kwa demokrasia ya nchi hiyo ni kuendelea kuwepo kwa siasa kali za mrengo wa kulia, huku akisema kuwa Wajerumani wanatakiwa kuzingatia hilo kabla ya kuvipigia kura vyama hivyo vyenye siasa kali za mrengo wa kulia. Faeser ameendelea kusema:

"Mwaka 2022, vitendo vya uhalifu vitokanavyo na misimamo mikali ya mrengo wa kulia viliongezeka kwa asilimia 3.8 hadi hadi kufikia 21,000. Pia, idadi ya watu wenye itikadi kali na wenye muelekeo wa vurugu imeongezeka mno kutoka watu 500 hadi 14,000 kwa sasa. Kamwe hatupaswi kupuuza tishio hili kubwa la itikadi kali na hata ugaidi wa mrengo mkali wa kulia."

Soma pia: AfD yajitenga na matamshi ya chuki kwa wahamiaji ya msemaji wake wa zamani

Lakini, kulingana na idara hiyo ya ujasusi, nadharia za msimamo mkali wa mrengo wa kushoto nazo pia zimeongezeka kwa 5.2% hadi kufikia watu 36,500 mwaka jana, huku baadhi ya watu hao wenye misimamo mikali ya mrengo wa kushoto wakiwa na mwelekeo wa vurugu. Hali hiyo inalinganishwa na karibu 14.5% ambayo ni takriban watu 38,800 wa mrengo wa kulia wenye mwelekeo wa vurugu.

Chama cha AfD ambacho hakikupenda kutoa maoni yake kwa sasa, kimekuwa kikijizolea wafuasi wengi nchini Ujerumani kutokana na sera yake ya kuzuia uhamiaji. Ukweli ni kwamba vyama vyenye misimamo mikali ya mrengo wa kulia vimekuwa vikijiimarisha kote barani Ulaya lakini kuibuka kwa chama cha AfD kunaibua hisia kutokana na historia mbaya ya Unazi ya Ujerumani.