1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Merkel, Macron wasaini mkataba wa Aachen kuifufua EU

Iddi Ssessanga
22 Januari 2019

Mwendelezo wa Mkataba wa Elysee ndiyo ishara ya karibuni ya urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani. Mkataba huo unaahidi ushirikiano wa karibu zaidi kati ya mataifa hayo na kusafisha njia ya mageuzi ya Umoja wa Ulaya.

https://p.dw.com/p/3BzLn
Angela Merkel und Emmanuel Macron unterzeichnen den neuen Elysée-Vertrag in Aachen
Picha: Getty Images/S. Schuermann

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na kansela wa Ujerumani Angela Merkel siku ya Jumanne walisaini mkataba mpya wa urafiki unaonuwiwa kuimarisha urafiki kati ya Ufaransa na Ujerumani, kupeleka uhusiano wao kwa ngazi mpya na kuboresha maisha ya raia wa mataifa yote mawili.

Mkataba huo ulisianiwa katika mji wa Ujerumani wa Aachen, wakati Ufaransa na Ujerumani zikiadhimisha miaka 56 ya Mkataba wa Elysee.

Wazo hilo siyo jipya. Paris hasa, imekuwa ikipendekeza mara kwa mara kusaini upya mkataba huo katika miongo kadhaa tangu uliposainiwa kwa mara ya kwanza, licha ya ukweli kwamba marekebisho yameongezwa katika muda wa miaka kadhaa.

Mkataba wa Aachen utakuwa "msingi wa ushirikiano baina ya mataifa yetu," alisema Merkel kabla ya hafla ya kusainiwa kwa mkataba mpya wa urafiki.

"Miaka 74, umri wa mtu, baada ya kumalizika kwa Vita kuu ya pili ya Dunia, kinachoonekana dhahiri ni kuhojiwa tena," alisema. Ndiyo maana, kwanza ya yote, kuna haja ya dhamira mpya kuelekea wajibu wetu ndani ya Umoja wa Ulaya, wajibu unaoshikiliwa na Ujerumani na Ufaransa."

Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron aliwakosoa wale "wanaoeneza uongo" kuhusu mkataba huo na kusisitiza umuhimu wa maridhiano ya Ufaransa na Ujerumani.

Angela Merkel und Emmanuel Macron unterzeichnen den neuen Elysée-Vertrag in Aachen
Rais wa Ufaransa Emmanuel Macron na Kansela wa Ujerumani Angela Merkel wakitia saini Mkataba wa Aachen Januari 22, 2019.Picha: Reuters/W. Rattay

"Wale wanaosahau thamani ya maridhiano kati ya Ufaransa na Ujerumani wanajigeuza kuwa washirika wa uhalifu wa wakati uliopita. Wale wanao...eneza uongo wanaumiza watu wale wanaojifanya kuwalinda kwa kutafuta kurudia historia yetu," alisema Macron.

Hata hivyo, waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Jean-Marc Ayrault aliiambia televisheni ya DW kuwa angependa kuuona mkataba wa Jumanne ukienda mbali zaidi.  "Haya siyo mapinduzi," alisema Ayrault. "Unaweza hata kusema kwamba ungeenda mbali zaidi - kudiriki zaidi."

Kutokana na ugumu wa kisiasa na kuibuka tena kwa siasa kali za kizalendo katika mataifa yote mawili, Ayrault alisema "tuna wajibu wa kudiriki. Huwezi kutaka makuu bila kudiriki. Hilo linakosekana kidogo. Hata kama naiona kuwa ni hatua chanya kwa ujumla."

Uhusiano ulioimarishwa

Mkataba wa awali ulisainiwa katika miaka ya 1960, miaka 18 tu baada ya kumalizika kwa Vita Kuu ya Pili ya Dunia. Januari 22, 1963, Rais wa Ufaransa Charles de Gaulle na Kansela wa Ujerumani Konrad Adenauer walisaini mkataba wa kihistoria wa Elysee uliohitimisha maridhiano kati ya mahasimu wakubwa wa zamani.

Kwa sahihi zao, serikali zilikubaliana juu ya mashauriano ya laazima, ushirikiano wa karibu wa kisiasa na mabadilishano mapana ya vijana. Tangu wakati huo, zaidi ya vijana milioni 8.4 wa Kijerumani na Kifaransa wameshiriki katika programu ya mabadilishano katika mataifa yote mawili.

Umuhimu wa Mkataba wa Elysee, ambao unaelezea tu mchakato wa ushirikiano, hauhitaji kubadilishwa - lakini mwendelezo huu mpya unanuwiwa kutuma ujumbe wa kisiasa, kwamba Berlin na Paris zinataka kushughulikia hatua inayofuata katika ushirikiano wa Ufaransa-Ujerumani na kuanda msingi wa mageuzi ya Umoja wa Ulaya. Wakati huohuo, urafiki ulioimarishwa zaidi unatazamwa kama njia ya kukabiliana na kuongezeka kwa siasa kali za kizalendo barani Ulaya.

Angela Merkel und Emmanuel Macron unterzeichnen den neuen Elysée-Vertrag in Aachen
Angela Merkel na Emmanuel Macron wakipeana mikono baada ya kusaini mkataba wa Aachen Januari 22, 2019.Picha: picture-alliance/dpa/O. Berg

Katika tangazo jipya la pamoja la kurasa 16, Merkel na Macron wamezungumzia mikakati katika maeneo mbalimbali ya kisera. Mkataba huo uliosainiwa upya unapanga kusogeza programu ya ubadilishanaji kwa raia wa nchi zote mbili na kuimarisha ushirikiano katika sera za Ulaya, nje na usalama. Pia unaahidi ushirikiano imara wa kiuchumi, ambao unahusisha sera zilizoratibiwa kuhusu mazingira na mabadiliko ya tabianchi. Hata hivyo sera za wakimbizi hazijashughulikia makhsusi.

Bunge la Ujerumani Bundestag na bunge la taifa la Ufaransa pia yemepitisha maazimio yanayotaka ushirikiano wa karibu kati ya mataifa yote mawili. Hii inahusisha mifano thabiti ambayo itatekelezwa sasa, kuanzia vituo vya pamoja vya mafunzo ya amali hadi kwenye vituo vya Ufaransa-Ujerumani kwa ajili ya teknolojia ya kisasa.

Zaidi ya hapo, makubaliano ya mabunge ya Ufaransa na Ujerumani yanatarajiwa kuimarisha mbadilishano kati ya mabunge mawili. Mipango hiyo pia inahusisha utekelezaji sawa wa maagizo ya Umoja wa Ulaya katika mataifa yote mawili.

Angalizo kwenye uchumi

Ujerumani tayari ndiyo mshirika muhimu zaidi wa kibiashara wa Ufaransa, lakini sasa mataifa hayo mawili yanapanga kusogea karibu zaidi pamoja na kuunda kanda ya kiuchumi ya Ufaransa-Ujerumani, na kupunguza ukiritimba.

"Kwa pamoja tuko bora kuliko kila mmoja wetu pekee yake - siyo tu kwenye soko la pamoja la ndani, lakini pia kwenye kanuni za pamoja katika sheria ya biashara, ufilisi na sheria za kampuni, na utaratibu sawa wa tathmini kwa ajili ya kodi za makampuni," Andrea Jung, mkuu wa kundi la wabunge wa Ufaransa-Ujerumani katika Bundestag aliiambia DW katika mahojiano.

Mwandishi: Iddi Ssessanga/DW

Mhariri: Grace Kabogo