1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaUbelgiji

Mataifa ya EU yajaribu kupata makubaliano kuhusu wahamiaji

4 Oktoba 2023

Wajumbe wa nchi 27 wanachama wa Umoja wa Ulaya wanakutana mjini Brussels wakitaraji kupata suluhisho la mkwamo kati ya Ujerumani na Italia

https://p.dw.com/p/4X6DJ
Meli ya uokozi baharini 'Humanity 1' ya shirika la Ujerumani ikiwa imewabeba wahamiaji 179 waliookolewa baharini Novemba 6, 2022. PICHA YA MAKTABA
Meli ya uokozi baharini 'Humanity 1' ya shirika la Ujerumani ikiwa imewabeba wahamiaji 179 waliookolewa baharini Novemba 6, 2022. PICHA YA MAKTABAPicha: Giovanni Isolino/AFP/Getty Images

Mkwamo huo unahusu meli za uokozi wa wahamiaji baharini. Maafikiano hayo yatawawezesha kuhitimisha makubaliano ya kugawana mzigo wa kuwahudumia wahamiaji. 

Kulingana na vyanzo vya habari, wajumbe hao wanakutana kujadili marekebisho ya makubaliano yaliyopendekezwa na Uhispania ambayo ni mwenyekiti wa mazungumzo hayo ya Umoja wa Ulaya hadi mwisho wa mwaka.

Mzozo kuhusu mashirika yasiyo ya serikali yanayowaokoa wahamiaji baharini, ulizuia upatikanaji wa makubaliano miongoni mwa mawaziri wa Uhamiaji wa Umoja wa Ulaya katika mkutano wao uliofanyika wiki iliyopita.

Viongozi wa nchi tisa za Mediterania wahimiza Umoja wa Ulaya kuchukua hatua kuzuia uhamiaji kwenye chanzo

Hata hivyo umoja huo ungali na lengo la kuafikiana kuelekea uchaguzi muhimu wa Ujerumani, Poland na wa bunge la Ulaya mwakani (2024).

Mkutano huo ni nafasi ya mwisho, kabla ya viongozi wa umoja wa kukutana kule Granada Uhispania Alhamisi na Ijumaa, ambapo watajadili uhamiaji kinyume cha sheria.

Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Ujerumani Nancy Faeser akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin Septemba 27, 2023.
Waziri wa Mambo ya Ndani nchini Ujerumani Nancy Faeser akizungumza na waandishi wa habari mjini Berlin Septemba 27, 2023.Picha: Maja Hitij/Getty Images

Haya yanajiri mnamo wakati kuna ongezeko la wahamiaji wanaotumia Bahari Mediterania kufika kisiwa cha Italia cha Lampedusa na kwingineko.Nchi kama Poland na Hungary zimeendelea kukataa kuwahifadhi wahamiaji wanaotoka Mashariki ya Kati na Afrika. Lakini umoja huo unaweza kupata makubaliano ambayo nchi hizo mbili pekee haziwezi kuzuia.

Takriban wahamiaji 300 wawasili Uhispania

Hayo yakijiri, wahamiaji wapatao 280 wamewasili katika visiwa vya Canary nchini Uhispania, baada ya kufunga safari hatari katika Bahari Atlantiki.

Shirika moja la uokozi limeliambia shirika la habari la AFP hayo na kuongeza kuwa hiyo ndiyo idadi kubwa ya wahamiaji kuwasili kisiwani humo wakiwa ndani ya boti moja.

Uhamiaji Umoja wa Ulaya bado suala tete

Kulingana na shirika hilo, miongoni mwa wahamiaji hao, 278 walikuwa wanaume, wavulana 10 na wanawake wawili, wote wakitokea kusini mwa jangwa la Sahara.

Ongezeko la wahamiaji wautia Umoja wa Ulaya wasiwasi
Ongezeko la wahamiaji wautia Umoja wa Ulaya wasiwasiPicha: Europa Press/ABACA/picture alliance

Kati ya mwezi Januari hadi Septemba 30 mwaka huu, takriban wahamiaji 15,000 wamewasili katika visiwa vya Canaries Uhispania. Hiyo ikiwa ni ongezeko la asilimia 19.8 ikilinganishwa na kipindi saw ana hicho mwaka uliopita. Hayo ni kulingana na takwimu za karibuni zaidi kutoka wizara ya ndani ya Uhispania.

Mashirika yasiyo ya serikali ya uokozi baharini mara kwa mara huripoti ajali za boti zinazosababisha vifo vya makumi na mamia ya wahamiaji katika maji makuu ya Morocco, Uhispania na kwingineko baharini.

Vyanzo: RTRE,AFPE