1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaIsrael

Marekani yakamilisha bandari ya misaada kwenye Pwani ya Gaza

Saleh Mwanamilongo
16 Mei 2024

Jeshi la Marekani limekamilisha ujenzi wa bandari ya muda kwa ajili ya kupeleka misaada kwenye Ukanda wa Gaza, licha ya kuendelea kwa mashambulizi ya Israel.

https://p.dw.com/p/4fuyk
Bandari ya muda, ambayo ilichukua wiki kukamilika, itatumika kama kitovu cha kupeleka misaada Gaza
Bandari ya muda, ambayo ilichukua wiki kukamilika, itatumika kama kitovu cha kupeleka misaada GazaPicha: GIUSEPPE CACACE/AFP via Getty Images

Kamandi Kuu ya jeshi la Marekani, CENTCOM, imesema Alhamisi kwamba bandari ya muda inayoelea itakayorahisisha kuingizwa misaada imekamilika kwenye pwani ya Ukanda wa Gaza.

Kwenye mtandao X,  zamani twitter, Kamandi hiyo ya jeshi la Marekani imesema malori yaliyobeba msaada wa kibinadamu yanatarajiwa kuanza kusonga mbele kwenye fukwe za pwani hiyo katika siku zijazo na kwamba Umoja wa Mataifa utapokea misaada na kuratibu shughuli ya usambazaji msaada Gaza.

Bandari ya muda, ambayo ilichukua wiki kukamilika, itatumika kama kitovu cha kupeleka misaada kwa vile Gaza yenyewe haina bandari ya kina cha kutosha kwa meli kubwa za mizigo.

Kulingana na taarifa za awali za wizara ya ulinzi ya Marekani, Pentagon, ni kwamba takribana malori 90 ya mizigo yataingia kwa siku Ukanda wa Gaza kupitia kituo hicho. Na baadae bandari hiyo itakuwa na uwezo wa kusafirisha malori 150 kwa siku. Misaada inayotarajiwa ni pamoja na chakula, maji na dawa.

Wanajeshi watano wa Israel wauawa 

Kwa upande mwengine, jeshi la Israel limesema kuwa wanajeshi wake watano wameuawa na wengine watatu kujeruhiwa kwa kupigwa risasi katika shambulizi la jeshi ambalo halikukusudiwa.

Wanajeshi hao waliuawa jana usiku katika eneo la kambi ya wakimbizi ya Jabalia kaskazini mwa Ukanda wa Gaza.

Wizara ya Afya ya Palestina pia imesema kuwa wanajeshi wa Israel wamewaua Wapalestina watatu katika Ukingo wa Magharibi wa Mto Jordan.

Mashambulizi Lebanon 

Wanajeshi watano wa Israel wauawa 'kimakosa' huko Jabalia
Wanajeshi watano wa Israel wauawa 'kimakosa' huko JabaliaPicha: Francisco Seco/AP/picture alliance

Huko Lebanon, vyombo vya habari vinavyomilikiwa na serikali ya nchi hiyo vimesema kuwa shambulizi la anga la Israel limefanywa usiku wa kuamkia leo mashariki mwa Lebanon. Shambulizi hilo limefanywa saa chache baada ya kundi la Hezbollah linaloungwa mkono na Iran kushambulia ndani kabisa ya ardhi ya Israel.

Hapo jana, jeshi la Israel lilitangaza kumuuwa mmoja wa makamanda wa Hezbollah katika shambulizi la kombora kusini mwa Lebanon.

Huku hayo yakijiri, Mahakama Kuu ya Haki ya Umoja wa Mataifa inatarajiwa kusikiliza kwa siku mbili kesi iliowasilishwa na Afrika ya Kusini ya kuitaka Israel kusitisha operesheni yake ya kijeshi katika mji wa Rafah.

Hii ni mara ya nne Afrika Kusini kuwasilisha ombi la aina hiyo kwenye Mahakama ya Kimataifa ya Haki kutaka hatua za dharura zichukuliwe ili kusitisha vita vya Israel huko Gaza.

Na baadaye leo, Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa limeitisha kikao kisicho rasmi kujadili hatma ya mateka wa Israel wanaoshikiliwa Gaza.