1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Maduro asema Venezuela haitasalimu amri kutokana na vitisho

Zainab Aziz Mhariri: Chilumba Rashid
13 Agosti 2021

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro amesema hatasalimu amri mbele ya vitisho baada ya Marekani kumwambia kwamba anapaswa kuitisha uchaguzi ikiwa anataka vikwazo dhidi ya nchi yake viondolewe.

https://p.dw.com/p/3yxgX
Venezuela Präsident Nicolas Maduro
Picha: Manaure Quintero/REUTERS

Maduro amesema hayo kabla ya mazungumzo kuanza nchini Mexico ambapo wawakilishi wa serikali yake  watakutana na wajumbe wa upinzani. Rais Maduro amesema nchi yake itashiriki kwenye mazungumzo hayo ikiwa huru na haitasalimu amri mbele ya vitisho au shinikizo la serikali ya Marekani.

Marekani imesema kiongozi huyo wa Venezuela anapaswa kufanya juhudi za dhati ili kuandaa uchaguzi wakati ambapo wawakilishi wa serikali yake wanatarajiwa kukutana na kiongozi wa upinzani Juan Guaido nchini Mexico anayezingatiwa na Marekani kuwa rais wa kipindi cha mpito. Marekani haimtambui Maduro kuwa rais halali wa Venezuela.

Rais wa Venezuela Nicolas Maduro
Rais wa Venezuela Nicolas MaduroPicha: Federico Parra/AFP/Getty Images

Mkutano huo ni wa matayarisho ya mazungumzo yanayopangwa kufanyika mwishoni mwa mwezi huu chini ya upatanishi wa Norway. Maduro ametaka kuondolewa mara moja alichoita vikwazo vyote vya kihalifu vilivyowekwa kwa maelekezo ya Marekani.

Msemaji wa wizara ya mambo ya nje ya Marekani Ned Price amewaambia waandishi habari kwamba utawala wa Maduro unaweza kufungua njia ya kulegezwa vikwazo kwa kuwaruhusu watu wa Venezuela kushiriki katika uchaguzi huru na wa haki uliopaswa kufanyika siku nyingi zilizopita. Msemaji huyo amesema kwa njia hiyo, utawala wa Maduro unalazimika kushiriki kwa dhati kwenye mazungumzo na kiongozi wa upinzani Juan Guaido yatakayoleta suluhisho kamili la mgogoro wa nchini Venezuela.

Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan Guaido
Kiongozi wa upinzani wa Venezuela Juan GuaidoPicha: Ariana Cubillos/AP Photo/picture alliance

Guaido alijitangaza kuwa rais wa Venezuala mnamo mwaka 2019 kutokana na wadhifa wake kama spika wa bunge. Rais wa Marekani wa hapo awali Donald Trump, akiwa na azma ya kuwachakaza wasoshalisti wote katika Amerika ya Kati aliweka vikwazo ili kumbana Maduro pia katika sekta ya mafuta, bidhaa kuu ya mauzo ya nchi za nje kwa Venezuela. Hata hivyo Maduro alilikabili shinikizo hilo kutokana na msaada wa jeshi lake na kutoka Urusi, China na Cuba.

Kwa mara ya mwisho Serikali ya Venezuela na wapinzani walifanya mazungumzo nchini Barbados mnamo mwaka 2019 pia chini ya upatanishi wa Norway. Hata hivyo hakuna kilichosonga mbele!

Vyanzo:/AFP/AP