1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Kansela Scholz azungumza na Rais Ruto

5 Mei 2023

Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani amekutana na kufanya mazungumzo na Rais William Ruto wa Kenya akiwa kwenye ziara yake barani Afrika kusaka mashirikiano zaidi kwenye masuala ya nishati jadidifu.

https://p.dw.com/p/4QweZ
Kenia | Bundeskanzler Olaf Scholz in Nairobi
Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Siku ya Ijumaa (Mei 5), Scholz aliwasili nchini Kenya na kukutana na kufanya mazungumzo na Rais wa Kenya William Ruto mjini Nairobi.

Scholz aliwasili Nairobi akitokea nchini Ethiopia, ambako aliunga mkono azma ya Afrika ya kuwa na kiti katika mkutano wa kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi lijulikanalo kama G20. 

Soma zaidi:Kansela Scholz ziarani Kenya

Katika ziara yake nchini Kenya Kansela Olaf Scholz anaambatana na viongozi kadhaa wa makampuni ya biashara kutoka Ujerumani.

Mjini Nairobi alipokelewa na Rais Ruto na mazungumzo ya kisiasa baina ya viongozi hao yalituama juu ya matumizi ya nishati endelevu, kupanua uhusiano wa kibiashara na utatuzi wa migogoro. 

Ujerumani kuunga mkono Afrika kwenye G20

Siku ya Alkhamis (Mei 5), Kansela huyo wa Ujerumani alitembelea makao makuu ya Umoja wa Afrika mjini Addis Ababa, ambapo alifanya mazungumzo na rais wa kamisheni ya umoja huo, Moussa Faki Mahamat.

Äthiopien | Bundeskanzler Scholz in Addis Abeba
Mwenyekiti wa Kamisheni ya Afrika, Mousa Faki Mahamat (kushoto), akiwa na mgeni wake Kansela Olaf Scholz wa Ujerumani mjini Addis Ababa.Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Katika mazungumzo hayo, Scholz alisema Afrika inapaswa kuwa na dhima kubwa zaidi katika masuala ya kimataifa, na aliahidi kuwa Ujerumani itaunga mkono matakwa ya Umoja wa Afrika kuwa katika mikutano ya kundi la G20.

Soma zaidi: Kansela Olaf Scholz awasili Kenya katika ziara yake Afrika

''Nimetoa tamko muhimu hapa katika Umoja wa Afrika. Tunataka kuunga mkono Umoja wa Afrika kupata kiti katika kundi la G20, ili uweze kushiriki na kuwa na kauli. Haya yanatokana na heshima kwa bara la Afrika, nchi nyingi za bara hilo, na idadi ya watu wake inayoongezeka.'' Alisema kansela huyo wa Ujerumani.

Pendekezo la Umoja wa Afrika kuwa na nafasi katika mikutano ya kundi la nchi zilizoendelea kiviwanda na zinazoinukia kiuchumi, G20, lilitolewa kwa mara ya kwanza na Rais Cyril Ramaphosa wa Afrika Kusini, na mara moja liliungwa mkono na Rais Joe Biden wa Marekani na Emmanuel Macron wa Ufaransa.

Kenya mfano mzuri kwa Afrika

Ujerumani ilikuwa nchi ya kwanza kuitambua Kenya kama jamhuri, baada ya kupata uhuru kutoka ukoloni wa Kiingereza.

Äthiopien | Bundeskanzler Scholz in Addis Abeba
Kansela Olaf Scholz akiwasili mjini Addis Ababa siku ya Alkhamis (Mei 4). Picha: Michael Kappeler/dpa/picture alliance

Wakati huu Berlin inaichukulia Kenya kama mshirika wake muhimu zaidi katika kanda ya Afrika Mashariki, na mfano mwema kwa uongozi wa kidemokrasia katika eneo hilo.

Soma zaidi: Kansela wa Ujerumani Olaf Scholz aelekea Ethiopia na Kenya katika ziara yake ya pili barani Afrika.

Siku ya Jumamosi (Mei 6), Kansela Scholz atakitembelea kiwanda cha kuzalisha nishati ya mvuke karibu na Ziwa Naivasha, kikubwa zaidi cha aina hiyo barani Afrika.

Makadirio tofauti yanaonesha kuwa kati ya asilimia 80 na 90 ya nishati inayotumiwa nchini Kenya inatokana na vyanzo endelevu, nchi hiyo ikiwa nambari tatu duniani katika sekta hiyo.

Vyanzo: dpa, Reuters