1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Idhaa ya Kiswahili ya DW yatimiza miaka 50

1 Februari 2013

Idhaa ya Kiswahili ya Deutsche Welle leo inaadhimisha miaka 50 tangu ilipoundwa na kuanza kurusha hewani matangazo yake hapo tarehe 1 Februari 1963 na kusikika katika maeneo ya Afrika Mashariki na Kati.

https://p.dw.com/p/17Kxp
Journalisten des DW Kisuaheli Teams in Studio in Köln (um 1960).
50 Jahre Kisuaheli RedaktionPicha: Conti-Press Heinz Fremke/Staatsarchiv Hamburg

Sherehe kubwa za kuadhimisha nusu karne hii zinafanyika kwenye makao makuu ya DW, Bonn, ambazo zinahudhuriwa na wageni kutokea sehemu mbalimbali wakiwemo mabalozi wa mataifa ya Afrika nchini Ujerumnai.

Hadi kufikia mwaka 1963, shirika la DW lilikuwa limeshatangaza kwa miaka 10 kwa kutumia lugha mbali mbali za Ulaya na halikutaka kulitelekeza bara la Afrika. Ndipo hapo wakuu wa shirika hili wakatafuta lugha kuu ya Kiafrika iliyokuwa ikizungumzwa katika eneo kubwa na Kiswahili kubahatika kuteuliwa hasa kutokana na uhusiano wa kihistoria uliokuwepo kati ya Wajerumani na wakazi wa Afrika Mashariki.

Wasomi wa Kijerumani pia walikuwa wakiongoza kwenye utafiti wa kiismu wa lugha ya Kiswahili. Padri wa Kijerumani Ludwig Krapf ndiye aliyeandika kamusi ya kwanza ya Kiswahili.

Tarehe 1 Februari 1963, Shirika la Utangazaji la DW lilizindua matangazo yake maalum ya lugha ya Kiswahili yaliyolilenga eneo la Afrika Mashariki na Kati.

Matukio muhimu duniani wakati huo

Rais John F. Kennedy akihutubia mjini Berlin tarehe 26 Juni 1963.
Rais John F. Kennedy akihutubia mjini Berlin tarehe 26 Juni 1963.Picha: picture alliance / akg-images

Matangazo hayo yalizinduliwa katika mwaka ambao ulikuwa pia na matukio maalumu ya kihistoria: hotuba ya kihistoria ya Rais wa Marekani J.F. Kennedy katika Berlin iliyogawanyika kwenye enzi za “Vita Baridi”. Wakati huo ndipo Kennedy alipotoa ile kauli yake maarufu “Ich bin ein Berliner”, yaani mimi ni Mberlin, kudhihirisha hisia zake za kuwaunga mkono Wajerumani waliokuwa wametenganishwa kutokana na ukuta uliokuwa umejengwa kuugawa mji wa Berlin.

Zanzibar nayo ilipata uhuru wake mwaka huo huo wa 1963 kutoka ukoloni wa Muingereza, sawa na taifa la Kenya, ambalo baada ya vita vikali vya kudai Uhuru, Rais wa kwanza wa Kenya huru, Jomo Kenyatta, akaingiya na kaulimbiu yake ya “Harambee”.

Nako nchini Ujerumani kwenye ulingo wa kisiasa mwaka huo wa 1963, Ludwig Erhard alichaguliwa kuwa kansela wa pili tangu Vita vya Pili vya Dunia vilipomalizika, akisisitiza juu ya Ujerumani moja. “Tunataka kuwania Ujerumani ambayo imeungana na ambayo itashirikiana na watu wote duniani.” Alisema Kansela Erhard.

Mwaka huo wa 1963 ndio mwaka ambao mpiganiaji haki za Wamarekani wenye asili ya Afrika, Martin Luther King, pamoja na wanaharakati wengine 250,000 walipoandamana kuelekea Washington. Martin Luther King alitoa hotuba yake maarufu iliyopewa jina la "Nina Ndoto", ambapo alisema: "Nina matumaini kwamba itafika siku ambapo watoto wa nchi hii watatathminiwa kwa tabia na hulka zao badala ya rangi ya ngozi”.

Idhaa ya Kiswahili ya DW hivi sasa

Sekione Kitojo (kushoto) na Mohammed Abdulrahman wakiwa kazini.
Sekione Kitojo (kushoto) na Mohammed Abdulrahman wakiwa kazini.Picha: DW

Turejelee matangazo yetu. Leo hii Idhaa ya Kiswahili ni mojawapo ya idhaa zilizopiga hatua zaidi kwenye matangazo ya Idhaa za DW. Tunatangaza kwa muda wa masaa matatu kila siku tukilenga maeneo ya Afrika ya Mashariki na Kati na eneo lote la Maziwa Makuu. Lengo letu ni lile lile: habari mpya zisizopendelea upande wowote na za kuaminika.

Sambamba na utangazaji, tunaendelea kuweka matangazo yetu kwenye mtandao na pia kwenye ukurasa wa Facebook. Tulikuwa idhaa ya kwanza ya kimataifa ya Kiswahili iliyoanzisha matumizi ya “iPhones” kwenye habari. Vyuo vikuu vingi vya Ulaya hivi sasa vinatumia ukurasa wetu kufundishia Kiswahili. Tunawatumia wasikilizaji na wasomaji wetu habari kwa ujumbe mfupi wa simu kila siku. Mtu anaweza kupata habari zetu pia kwenye Twitter. Huwa pia tunawatumia wasomaji wetu kijarida cha habari kupitia barua-pepe.

Waandishi na watangazaji wetu kutoka katika nchi tano za Afrika Mashariki na Kati hushirikiana na waandishi wengine wengi walioko kwenye maeneo mbalimbali Afrika na duniani kwa ujumla. Kuna makala za aina mbali mbali kuanzia siasa, haki za binadamu, mazingira, wanawake na maendeleo, vijana, afya na utamaduni.

Daima tumekuwa tukizingatia habari huru na zisizoelemea upande wowote na pia maingiliano mema ya kitamaduni.

Idhaa ya Kiswahili ya DW imekuwa ikitangaza kupitia masafa mafupi kwa kipindi chote hiki cha miaka 50, lakini pia kutokana na ushirikiano kati yetu na vituo vingine vya utangazaji nchini Tanzania, Jamhuri ya Kidemokrasia ya Kongo, Uganda, Rwanda, Burundi na Kenya, tunaweza kukutangazia kwa kina yale yanayotukiya Afrika na ulimwenguni kote kupitia vituo vya redio za FM.

Tunavishukuru sana vituo vyote tunavyoshirikiana navyo kwa kuwa ni washirika wa kutegemewa. Tunajitahidi kuhakikisha kwamba tunawaletea taarifa za uhakika na zisizoelemea upande wowote.

Kwa hakika, tunafurahia jinsi munavyoyapokea matangazo yetu na ujumbe, barua na maoni mbalimbali kuhusu matangazo haya.

Mimi pamoja na kundi zima la watangazaji wa Idhaa ya Kiswahili ya DW tunawashukuru kwa kusikiliza matangazo yetu na kuwa mashabiki wetu waaminifu.

Mwandishi: Andrea Schmidt, Mkuu wa Idhaa ya Kiswahili ya DW

Mhariri: Mohammed Khelef