1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

G7 'tayari kuichukilia Iran hatua' kwa kuiyumbisha kanda

Bruce Amani
15 Aprili 2024

Viongozi wa nchi saba tajiri duniani - G7 wameonyesha uungaji mkono wao kamili kwa Israel kufuatia shambulizi la Iran, na kusema wako tayari kuchukua hatua zaidi katika kujibu walichoita mipango zaidi ya kuyumbisha.

https://p.dw.com/p/4ekpz
Droni za Iran
Iran ilirusha mamia ya droni kuelekea Israel kulipiza kisasi shambulizi lililofanywa kwenye ubalozi wake mdogo DamascusPicha: Iranian Army Office/ZUMA Wire/IMAGO

Katika taarifa kufuatia mkutano wa video, viongozi hao wa G7 walisema wanalaani vikali shambulizi la moja kwa moja na lisilo la kawaida la Iran dhidi ya Israel. Mataifa hayo yameitaka Iran na washirika wake kusitisha mashambulizi yao.

Rais wa Halmashauri Kuu ya Ulaya Ursula von der Leyen amesema katika taarifa tofauti kuwa katika kwenda mbele, watatafakari vikwazo zaidi dhidi ya Iran kwa ushirikiano wa karibu na washirika wao, na hasa kuhusu mipango ya nchi hiyo ya droni na makombora.

Iran yarusha droni kuelekea Israel
Mifumo ya ulinzi wa angani ya Israel iliziharibu mamia ya droni ilizorushwa na Iran Picha: Atef Safadi/EPA

Iran ilifanya shambulizi, lake la kwanza la moja kwa moja kwenyse ardhi ya Israel, katika kulipiza shambulizi kali la angani lililodaiwa kufanywa na Israel na kuharibu jengo la ubalozi wake mdogo katika mji mkuu wa Syria Damascus mapema mwezi huu. Shambulizi hilo lilijiri wakati vita kati ya Israel ha Hamas vikiendelea huko Gaza.

UN yaonya dhidi ya kulipiza kisasi

Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterress ameuambia mkutano wa Baraza la Usalama kuwa watu wa mashariki ya Kati wanakabiliwa na hatari ya kweli ya kuzuka mgogoro kamili na sasa ni wakati wa kuituliza mivutano. Ametoa ombi la pande zote kujizuia kufuatia mashambulizi ya Iran dhidi ya Israel. Aidha aliwaonya wanachama wote wa Umoja wa Mataifa kuwa hatua yoyote ya kulipiza kisasi kwa nguvu itakuwa kinyume cha sheria chini ya sheria za kimataifa.

Balozi wa Iran Amir Saeid amerudia madai ya Tehran kuwa ilichukua hatua hiyo ili „"kujilinda" baada ya mlipuko wa Aprili mosi katika ubalozi wake mdogo wa Damascus, ambalo Iran iliilaumu Israel.

Mkutano wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa
Katibu Mkuu wa Umoja wa Mataifa amesema Mashariki ya Kati iko kwenye ukingo wa kutumbukia katika mgogoro kamiliPicha: Fatih Aktas/Anadolu/picture alliance

Amir amekiambia kikao cha Jumapili kuwa Baraza la Usalama lilishindwa katika wajibu wake wa kudumisha amani na usalama wa kimataifa baada ya mlipuko huo. Kwa hiyo Jamhuri ya Kiislamu ya Iran haikuwa na chaguo jingine bali kujibu na akaelezea jibu hilo kuwa lililostahili na la kiwango kinachofaa.

Israel yasema Iran lazima ilipie kitendo hicho

Balozi wa Israel katika Umoja wa Mataiga Gilad Erdan aliituhumu Iran kwa kukiuka sheria za kimataifa kwa kufanya shambulizi hilo. Amelitolea wito baraza hilo lenye nchi wanachama 15 kuilaani Iran, kuiwekea upya vikwazo na kuorodhesha vikosi vya Walinzi wa Mapinduzi wa Iran kuwa shirika la kigaidi.

Naibu balozi wa Marekani katika Umoja wa Mataifa Robert Wood alilihimiza Baraza la Usalama kulaani shambulizi hilo la Iran. Alisema katika siku zijazo, na kwa ushirikiano na mataifa mengine wanachama, Marekani itatafakari hatua za ziada za kuiwajibisha Iran katika Umoja wa Mataifa.

Vyanzo: mashirika