1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW
SiasaArmenia

Bunge la Armenia laidhinisha nchi hiyo kujiunga na ICC

3 Oktoba 2023

Bunge la Armenia limepiga kura kuidhinisha nchi hiyo kujiunga na Mahakama ya Kimataifa ya Uhalifu wa Kivita, ICC, kiasi wiki moja tangu jirani yake Azerbaijan ichukue udhibiti wa jimbo la Nagorno Karabakh.

https://p.dw.com/p/4X4rE
Kikao cha Bunge öa Armenia mjini Yerevan
Wabunge wa Armenia wakihudhuria kikao kilichopitisha uamuzi wa nchi yao kujiunga na Mahakama ya ICC.Picha: Hayk Baghdasaryan/AP Photo/picture alliance

Katika kura iliyopigwa leo mchana, wabunge wa Armenia wameidhinisha mkataba wa Roma uliounda mahakama ya ICC kwa kura 60 za waliounga mkono dhidi ya 22 walioupinga.

Uamuzi huo unafungua njia kwa taifa hilo la Asia ya Kati kujiunga na mahakama hiyo yenye makao yake huko The Hague, Uholanzi yenye dhima ya kuchunguza na kuendesha kesi za makosa ya kivita na uhalifu dhidi ya ubinadamu.

Armenia ilikuwa na dhamira ya kujiunga na ICC kiasi miaka 20 iliyopita lakini mchakato huo ulisimama baada ya mahakama ya taifa hilo kusema mkataba ulioanzisha mahakama ya ICC unakiuka katiba ya Armenia.

Tangu wakati huo katiba ya nchi hiyo imefanyiwa marekebisho mara mbili na mwezi Machi mwaka huu uamuzi ulitolewa kuwa katiba ya sasa inaweza kuiruhusu Armenia kujiunga na ICC.

Dhamira ya kujiunga na ICC ni kutokana na mvutano na Azerbaijan? 

Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan (kushoto) na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan.
Rais Ilham Aliyev wa Azerbaijan (kushoto) na Waziri Mkuu wa Armenia Nikol Pashinyan. Picha: GENT SHKULLAKU/AFP

Mjumbe wa Armenia kuhusu masuala ya kisheria kwa ngazi ya kimataifa Yegishe Kirakosyan amekaririwa akisema dhamira hasa ya nchi hiyo kuanza tena mchakato huo imechochewa na kile serikali ya nchi hiyo imekitaja kuwa uhalifu uliofanywa na jirani yake Azerbaijan kwenye mzozo wa kuwania jimbo la Nagorno Karabakh.

Serikali mjini Yerevan inaituhumu Azerbaijan kuwauwa wafungwa wa Kiarmenia na inataka mahakama ya ICC iwe na nguvu ya kuchunguza matukio ya kuanzia mwezi Mei mwaka 2021.

Hata hivyo uwezekano wa ICC kuchunguza makosa yanayodaiwa kutendwa kabla ya Armenia kuwa mwanachana ni suala linatarajiwa kuwa na mchakato mrefu kisheria.

Lililo wazi lakini ni kwamba uamuzi huo wa leo ni msumari mwingine kwenye mahusiano yaliyodorora kati ya Armenia na mshirika wake Urusi, ikitiliwa maanani kuwa mahakama ya ICC imetoa waranti wa kukamatwa kwa rais Vladimir Putin.

Kremlin: Uamuzi wa Armenia unazusha maswali mengi kutoka Moscow 

Msemaji wa ikulu ya Kremlin, Dmitry Peskov, amesema uamuzi huo wa Armenia siyo sahihi na unazusha maswali mengi kuhusu mshirika wake huyo muhimu kwenye kanda hiyo.

Jeshi la Azerbaijan wakati wa vita na Armenia mwaka 2020.
Azerbaijan na Armenia zimepiga vita mbili kuwania jimbo la Nagorno-Karabakh.Picha: Azerbaijan's Defense Ministry/AP Photo/picture alliance

Yafaa kukumbusha hapa kuwa Urusi ni mshirika wa karibu wa Armenia na Azerbaijan, mataifa mawili jirani yaliyokuwa sehemu ya Dola ya Kisovieti na yaliyotumbukia kwenye mzozo wa kuwania jimbo la Nagorno Karabakh kwa miaka 30.

Armenia yenyewe inasema imefadhaisha na msimamo uliochukuliwa na Urusi juu ya mzozo wa Nagorno Karabakh kwa serikali mjini Moscow kuipendelea Azerbaijan na kwamba inahisi kutengwa na dola hiyo.

Madai hayo lakini yanapingwa na msemaji wa Kremlin, Dmirty Peskov.

"Kuhusu suala la Karabakh lazima tukumbuke uamuzi wa waziri mkuu wa Armenia alioufikia mjini Prague wa kutambua mipaka ya Azerbaijan ya mwaka 1991. Aliitambua kuwa Karabakh ni eneo la Azerbaijan. Na huo ukawa msingi wa yote yanayotokea sasa." amesema Afisa huyo wa utawala wa Urusi.

Mataifa ya Ulaya yatafakari mahusiano na Azerbaijan baada ya kuitwaa Karabakh 

Msururu wa magari uliowabeba Waarmenia wanaolikimbia jimbo la Nagorno-Karabakh
Msururu wa magari uliowabeba Waarmenia wanaolikimbia jimbo la Nagorno-Karabakh Picha: Irakli Gedenidze/REUTERS

Misuguano yote hiyo imezidi makali tangu Azerbaijan ilipochukua udhibiti wa jimbo la Karabakh zaidi ya wiki moja iliyopita na kusababisha maelfu ya wakaazi wa jimbo hilo wenye asili ya Armenia kulikimbia.

Hapo jana basi la mwisho lililowabeba Waarmenia liliondoka Karabakh na kuhitimisha wiki nzima ya kuhama zaidi ya wakaazi 100,000 wenye asili ya Armenia kutoka jimbo hilo.

Mataifa ya magharibi yamechukua upande wa Armenia kwenye mvutano huo wa sasa juu ya hadhi ya jimbo la Karabakh.

Mapema hii leo nyaraka rasmi za Umoja wa Ulaya zimefichua dhamira kuwa kanda hiyo inaweza kupitia upya mahusiano yake na Azerbaijan ikiwa ni pamoja na kuinyima misaada iwapo hali ya kiutu kwenye jimbo la Karabakh itazidi kuwa mbaya.

Umoja huo kwa kauli moja tayari ulishakosoa operesheni ya Azerbaijan iliyofanikisha kulikamata kikamilifu jimbo la Karabakh ambalo chini ya sheria ya kimataifa ni sehemu ya ardhi yake lakini ilikuwa inakaliwa na jamii kubwa ya watu wenye asili ya Armenia.