1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Biden alaani visa vya ubaguzi wa rangi

29 Agosti 2023

Rais wa Marekani Joe Biden ametoa wito wa kukomeshwa kwa mauaji yanayochochewa na chuki dhidi ya watu weusi na kusisitiza kuwa kukaa kimya kunachukuliwa kama kuunga mkono mauaji ya aina hiyo.

https://p.dw.com/p/4VgIZ
Rais Joe Biden akiwa kwenye mkutano na familia ya mwanaharakati Martin Luther King
Rais Joe Biden akiwa kwenye mkutano na familia ya mwanaharakati Martin Luther KingPicha: Susan Walsh/AP Photo/picture alliance

Rais Biden ameyasema hayo katika maadhimisho ya miaka 60 ya kumbukumbu ya matembezi ya "March on Washington" yaliyoongozwa na mwanaharakati wa kupigania haki za kiraia Marthin Luther King.

Katika hotuba ya kihistoria ya "Nina Ndoto," mwanaharakati huyo aliihimiza serikali ya Marekani kuhakikisha haki sawa kwa watu weusi.

Wito wa Biden ameutoa baada ya mwanamume mzungu mwenye umri wa miaka 21 kuwashambulia kwa risasi na kuwauwa watu watatu weusi kwenye duka moja liitwalo Dollar General mwishoni mwa juma.

Mkuu wa polisi wa Jacksonville alisema kuwa shambulio hilo lililochochewa na chuki dhidi ya watu weusi.

Hata hivyo, hakuna ushahidi wowote kwamba mshukiwa alikuwa sehemu ya kundi lolote.

Makamu wa rais Kamala Harris, Mmarekani wa kwanza mweusi kuchaguliwa katika nafasi hiyo, pia alikuwemo kwenye mkutano huo na kusema kwamba, Wamarekani wana mengi zaidi ya kuwaunganisha tofauti na yanayowatenganisha.