1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Azimio la Nairobi la hali ya hewa kutiwa saini

Tatu Karema
6 Septemba 2023

Mazungumzo ya kihistoria ya hali ya hewa barani Afrika yanatarajiwa kuhitimishwa Jumatano ( 6.09.2023) nchini Kenya huku viongozi wakitafuta azimio la pamoja kuangazia uwezo wa bara hilo wa matumizi ya nishati jadidifu

https://p.dw.com/p/4W0MO
Rais wa Kenya William Ruto atoa hotuba wakati wa ufunguzi wa mkutano wa kilele wa hali ya hewa barani Afrika jijini Nairobi nchini Kenya mnamo 4.09.2023
Rais wa Kenya William Ruto ahutubia mkutano wa kilele wa hali ya hewa barani AfrikaPicha: Monicah Mwangi/REUTERS

Azimio hilo la Nairobi linanuia kuweka mfumo wa mwelekeo wa vitendo kukuza sekta ya nishati mbadala na kuongeza ufadhili wa ulinzi wa hali ya hewa kwa mataifa ya Afrika. Maafisa wanasema, kulingana na takwimu, Afrika inahusika na ongezeko la viwango vya chini vya joto la chini ya asilimia 4 lakini inalipa gharama ya juu.

Azimio latafuta suluhu ya mzigo wa madeni barani Afrika

Azimio hilo la mwisho kutoka mkutano huo wa Nairobi linatarajiwa kutoa wito kwa jamii ya kimataifa kusaidia kupunguza mzigo mkubwa wa madeni kwa Afrika na kurekebisha mfumo wa kifedha wa kimataifa kuwezesha uwekezaji.

Soma pia:Guterres aurai ulimwengu kuisaidia Afrika kuwa mzalishaji mkubwa wa nishati jadidifu

Akizungumza wakati wa mkutano huo, rais wa Kenya William Ruto amesema kuwa sababu kubwa ya mzigo mkubwa wa madeni barani Afrika ni viwango vya juu vya riba na kwamba bara hilo linalipa mara tano zaidi ikilinganishwa na mabara menine. Ruto amesema hali hiyo inamaanisha kuwa mpangilio umewekwa katika hali kwamba unapo kopa, inakuwa vigumu kulipa deni hilo.

Viongozi wa Afrika wanalitazamia bara hilo kun'gara katika jukwaa la kimataifa

Ruto ameongeza kuwa viongozi wa Afrika wanatazamia siku za usoni ambapo bara la Afrika hatimaye litaingia katika jukwaa la kimataifa kama nguvu ya kiuchumi na kiviwanda . Viongozi hao pia watatoa wito kwa mataifa yanayochangia zaidi utoaji wa hewa chafu kutimiza ahadi zao za muda mrefu kuhusu hali ya hewa kwa mataifa maskini.

Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio Guterres akihutubia mkutano wa kilele wa hali ya hewa barani Afrika jijini Nairobi nchini Kenya mnamo 5.09.2023
Katibu mkuu wa Umoja wa Mataifa Antonio GuterresPicha: Luis Tato/AFP

Soma pia:Ruto asema mabadiliko ya tabianchi yanatafuna maendeleo ya Afrika

Wachambuzi wanasema umoja huenda ukachangia kasi ya mfululizo wa mikutano muhimu kuelekea mkutano wa kilele wa Umoja wa Mataifa kuhusu hali ya hewa unaoanza mwezi Novemba, ukiwemo mkutano wa G20 wikendi hii.

Kuna changamoto katika kuafikia makubaliano barani Afrika

Lakini makubaliano yanaibua changamoto katika bara hilo lenye idadi ya watu bilioni 1.4 ambapo baadhi ya serikali zinapigia upatu nishati mbadala huku nyingine zikitetea hifadhi zao za nishati ya kisukuku.

Soma pia:Viongozi wa Afrika wakutana kujadili mazingira Nairobi

Kenya imekuwa katika mstari wa mbele katika nishati jadidifu na kuahidi kwamba itatumika kwa asilimia 100 katika umeme wake kufikia mwaka 2030.

Umoja wa Falme za Kiarabu wapiga jeki ufadhili katika nishati jadidifu

Juhudi za mkutano huo za kuongeza ufadhili katika nishati jadidifu pia zilipigwa jeki hapo jana baada ya Umoja wa Falme za Kiarabu kuahidi dola bilioni 4.5 kuongeza kasi ya bara Afrika katika matumizi ya nishati safi. Mkutano huo wa siku tatu ulihudhuriwa na viongozi wa mataifa ya Afrika, wawakilishi wa Umoja wa Mataifa na maafisa kutoka mashirika mengine ya kiserikali na yasiokuwa ya kiserikali pamoja na sekta ya kibinafsi.