1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Askofu Tutu aagwa na wakazi wa Afrika Kusini

Lilian Mtono
30 Desemba 2021

Raia nchini Afrika Kusini wamemiminika katika kanisa la Mtakatifu George lililopo kwenye mji wa Cape Town hii leo kutoa heshima zao za mwisho kwa aliyekuwa Askofu mkuu wa kanisa la Anglikana nchini humo Desmond Tutu.

https://p.dw.com/p/44zpE
Südafrika Kapstadt Trauer um Desmond Tutu
Watu nchini Afrika Kusini wameendelea kuomboleza tangu mpigania haki huyo alipofariki Disema 24. Picha: AP/picture alliance

Makasisi sita wa kanisa la Anglikana walilibeba jeneza lililokuwa na mwili wa Askofu mkuu Desmond Tutu,  hadi kwenye kanisa la Mtakatifu George ambako mwili wake ulilazwa. Jeneza lake lilikuwa ni la kawaida kabisa lililotengenezwa kwa mti wa msonobari na kupambwa kwa shada moja tu la maua meupe.

Kulingana na wakfu wa Askofu Tutu mshindi wa tuzo ya Amani ya Nobel, mwenyewe hakutaka makuu kwenye mazishi yake na kusema mwanaharakati huyo aliomba hata jeneza lake liwe la bei ya chini kabisa. Aliagiza pia heshima za kijeshi zitolewe kwa kiasi. Mkewe Leah atakabidhiwa bendera ya Afrika Kusini.

Soma Zaidi: Ta'azia: Askofu Mkuu Desmond Tutu, mwanaharakati asiyechoka

Mchungaji Gilmore Fry ameliambia shirika la habari la AFP mapema leo kwamba mwili wa Askofu Tutu utakuwa mahali hapo kwa siku mbili ili kuepusha mkanyagano ambao unaweza kutokea, kwa kuwa wanataka kuruhusu watu wengi iwezekanavyo kumuaga kwa mara ya mwisho mpambanaji huyo ambaye hakuchoka kupigania haki za weusi nchini Afrika Kusini na kusimamia maridhiano.

Askofu mkuu Desmond Tutu alifariki Disemba 24, akiwa na miaka 90. Na baada ya shughuli ya kumuaga kukamilika, mwili wake utachomwa moto na majivu yatazikwa Jumamosi siku ya mwaka mpya. Shughuli ya mazishi itakuwa ndogo tu kama alivyoagiza mwenyewe kabla ya kifo chake.

Flash-Galerie Desmond Tutu
Askofu Desmond Tutu alifariki dunia Disemba 24, 2021Picha: AP

Mtoto wa rais wa kwanza mweusi nchini humo Nelson Mandela, Mandla Mandela ambaye pia ni mbunge wa bunge la kitaifa ametoa heshima zake hii leo, na kusema ilikuwa ni heshima kubwa kumuaga askofu Tutu ambaye kampeni zake zilisaidia kuuondoa utawala wa kikatili na kuleta demokrasia.

Tizama Albamu ya Picha: Vifo vya watu maarufu vilivyotokea 2021

Wakazi wa Afrika Kusini wasema watamkumbuka Askofu Tutu kwa mengi.

Kabla jeneza lake halijafunguliwa kwa watu kumuaga, kanisa lilifanya ibada iliyohudhuriwa na wanafamilia, ikiwa ni pamoja na mjane wake Leah. Na hatimaye raia wa Afrika Kusini walianza kumuaga na miongoni mwao wakazungumza na vyombo vya habari.

Johan Magerman "Tumekuja hapa kuonyesha masikitiko yetu makubwa kutokana na kifo cha askofu. Alikuwa mtu wa imani, tuliyempenda sana. Alikuwa shujaa wa kweli, kwa hiyo tukaona angalau tuonyeshe sehemu yetu ya heshima." Pamoja naye ni Marilyn Jones, aliyesema "Niko hapa kutoa heshima za mwisho kwa mtu huyu wa kuheshimiwa.Tutamkumbuka tu kwa upendo wake na namna alivyozungumzia kwa uwazi mema na mabaya."

Lakini, hata kabla ya leo, mamia ya watu tayari walianza kumiminika kwenye kanisa hilo la Mtakatifu George tangu siku ya Jumapili, ambako Tutu alihudumu kama askofu mkuu kwa muongo mmoja hadi mwaka 1996, wakiweka maua na kusaini kitabu cha maombolezo, wakati taifa hilo likiadhimisha wiki ya maombolezo na bendera ikipepea nusu mlingoti.

Katika miaka ya karibuni, askofu Tutu aliamua kuachana na shughuli za umma kutokana na afya yake kudhoofishwa na saratani ya tezi dume. Amemuacha mkewe Leah walioana tangu mwaka 1955 na wana watoto wanne. Mungu ailaze mahala pema peponi roho ya marehemu Askofu Mkuu Emeritus Desmond Tutu. Amen.

Tizama Zaidi: 

Maisha na urithi wa Askofu Desmond Tutu

Mashirika: RTRE/AFPE