1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Mataifa sita yenye nguvu yaijadili Iran.

Halima Nyanza15 Aprili 2010

Wanadiplomasia kutoka katika mataifa sita yenye nguvu duniani wamesema mkutano wao uliofanyika jana Jumatano juu ya kuiwekea Iran vikwazo vipya, ili kujaribu kuifanya iachane na mpango wake wa nyuklia umetoa matumaini.

https://p.dw.com/p/Mwis
Rais wa Iran Mahmoud Ahmadinejad, nchi yake inalaumiwa kwa mradi wake wa nyuklia.Picha: AP
Mabalozi kutoka katika nchi tano wanachama wa kudumu wa Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa pamoja na Ujerumani walikutana katika makao Makuu ya Umoja wa Mataifa mjini New York katika mkutano wao wa pili katika kipindi cha wiki, tangu China, ambayo inauhusiano wa karibu wa kiuchumi na Iran, kukubali kujiunga katika mazungumzo hayo. Wanadiplomasia hao walikuwa wakijadiliana juu ya azimio la awali, ambalo lilisambazwa wiki zilizopita, linaloandaa kuweka awamu ya nne ya vikwazo dhidi ya Iran kutokana na kukataa kwake kuachana na mpango wake wa kurutubisha nyuklia. Akizungumzia na waandishi wa habari mara tu baada ya mkutano wao huo uliochukua saa 3, balozi wa Ufaransa Gerard Araud amesema wamefikia katika hoja ya msingi, hali inayowafanya kusonga mbele na kufahamisha pia kwamba watafanya mikutano mingine. Hata hivyo hakufahamisha mkutano ujao utafanyikiwa wapi. Naye balozi wa China Li Baodong ameelezea kuafikiana zaidi katika mkutano huo. Nchi za magharibi zimekuwa zikiiilaumu Iran kwamba inataka kutengeneza silaha za nyuklia, lakini Iran yenyewe inasema kuwa lengo la nyuklia hiyo ni kuzalisha umeme kwa ajili ya matumizi ya raia. Muswada huo ulioandaliwa na Marekani unapendekeza hatua mpya za kuzibana benki za Iran, nchi hiyo kuwekewa vikwazo kamili vya silaha, hatua kali dhidi ya biashara ya nchi hiyo ya kusafirisha kwa meli, kupigwa marufuku kwa vitega uchumi vipya katika sekta ya nishati ya Iran na pia hatua dhidi ya askari wa kikosi cha mapinduzi cha nchi hiyo. Katika mkutano wa kwanza uliofanyika Alhamisi iliyopita, ambao pia ulihudhuriwa na mabalozi kutoka nchi hizo sita, Marekani, Uingereza, Ujerumani, Ufaransa na Urusi, balozi wa China Li Baodong alioneshwa kukwera na maependekezo hayo ambayo yanaathiri sekta ya nishati ya Iran. Rais Barack Obama wa Marekani amezishinikiza nchi zilizohudhuria mkutano  juu ya usalama wa nyuklia mjini Washington siku ya Jumanne kuiwekea vikwazo Iran  lakini alikiri kuwa China ina wasiwasi juuu ya madhara ya kiuchumi na kusema kwamba majadiliano ni magumu. Mataifa ya magharibi yamekuwa yakisema kuwa uchu wa Iran kupata silaha za nyuklia utaweza kuyumbisha  kwa kiasi kikubwa eneo hilo la mashariki ya kati. Mwandishi: Halima Nyanza(Reuters) Mhariri: Mohammed, Abdul-Rahman