1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Waziri mkuu Netanyahu akutana na Rais Sarkozy

12 Novemba 2009

Asema yuko tayari kuzungumza na Rais Assad wa Syria

https://p.dw.com/p/KUY8
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu.Picha: picture-alliance/ dpa

Waziri Mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amekutana na Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa kwa mazungumzo juu ya mgogoro ulioko kwenye mchakato wa amani Mashariki ya Kati na inaonekana kwamba amefunguwa milango kwa mazungumzo na Syria.

Hata hivyo mkutano huo wa jana (Jumatano) mjini Paris hakuonyesha dalili ya kupiga hatua yoyote ile ya maendeleo juu ya suala la amani kati ya Israel na Wapalestina .

Viongozi hao wawili hawakuzungumza na waandishi wa habari baada ya mkutano wao wa masaa mawili katika Kasri la E´lysee na Netanyahu aliondoka kurudi nyumbani muda mfupi baada ya mkutano huo.

Taarifa fupi kutoka ofisi ya Sarkozy imesema kwamba mazungumzo hayo yaliwajumuisha viongozi hao na kila akiwa na mshauri wake mmoja tu mwandamizi.

Schweiz ILO Internationale Arbeits Organisation in Genf - Nicolas Sarkozy Präsident Frankreich
Rais wa Ufaransa Nikolas Sarkozy.Picha: AP

Walijadili masuala ya kimataifa na hususan njia za kuanza upya mchakato wa amani Mashariki ya Kati.

Wakati hali ya mkutano huo haikuwekewa matumaini makubwa afisa serikali ya Israel ameweka nafasi ya mojawapo ya njia ya mazungumzo kwa mapango huio wa amani uliokwama.

Syrien Präsident Baschar al-Assad
Rais Hafidh al-Assad wa SyriaPicha: picture-alliance/ dpa

Mshauri huyo mwandamizi amesema Sarkozy alilitaja suala la amani na Syria na kwamba Waziri Mkuu Netanyahu yuko tayari kukutana na Rais wa Syria wakati wowote ule na mahala popote pale kusonga mbele na mpango huo wa amani lakini bila ya masharti yoyote yale.

Kwa mujibu wa shirika la habari la SANA nchini Syria mapema Rais Bashar al Assad wa Syria ameuambia mkutani wa wanasiasa mjini Damascus kwamba Syria haitoweka masharti ya kufikiwa amani lakini ameonya kwamba ina haki zake ambazo hawatozikana.

BdT Baustelle Siedlungen in der West Bank
Eneo moja wapo la ujenzi wa makaazi ya Wayahudi karibu na Jerusalem.Picha: AP

Assad anatazamiwa kuwasili Paris hapo kesho (Ijumaa) kwa mazungumzo na Sarkozy.

Israel iliiteka Milima ya Golan kutoka Syria katika Vita vya Mashariki ya Kati vya mwaka 1967 na kuitwaa kabisa hapo mwaka 1981.Serikali ya Syria imekuwa ikidai mara kwa mara kwamba kurudishwa kwa milima hiyo ni sharti lisilokuwa na mjadala kwa ajili ya amani.

Katika suala la amani kati ya Israel na Wapalestina akizungumza katiika mkesha wa ziara ya Netanyahu waziri wa mambo ya nje wa Ufaransa Bernard Kouchner amesema tafauti ya kweli ya kisiasa inayomtenganisha Sarkozy na Netanyahu ni suala la Israel kuendelea na ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina.

Amesema kwamba kusitishwa kwa ujenzi wa maakazi hayo kusema kwamba hakuna tena kuendeleza ukoloni wakati mazungumzo yakiendelea litakuwa ni jambo lisiloweza kuepukwa kabisa.

Hofu ya Ufaransa kwa machakato wa amani imezidi kuongezeka kutokana na Rais Mahmoud Abbas wa Wapalestina kutishia kujiuzulu kupinga kushindwa kwa Marekani kuibinya Israel isitishe hatua yake ya kuendelea na ujenzi wa makaazi hayo katika ardhi ya Wapalestina katika Ukingo wa Magharibi.

Akihutubia mkutano wa hadhara wa kumbukumbu ya miaka mitano tokea kufariki kwa Yasser Arafat mjini Ramallah hapo jana Abbas amesema mazungumzo ya amani na Israel lazima yazingatie hadidu za rejea za amani na hiyo inaamanisha lazima isitishe ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina.

Amesema msingi wa mazungumzo hayo ya amani ni kuzingatia maazimio ya Umoja wa Mataifa ya kurudi katika mipaka ya Israel iliokuwepo mwaka 1967 katika mkesha wa mzozo huo ambao umebadili ramani ya Mashariki ya Kati.

Abbas anaonekana kwa wengi kuwa ni kiongozi pekee wa Wapalestina mwenye madaraka na kuweza kuaminika kufanikisha mazungumzo ya maana na kundoka kwake kunaweza hata kukachochea kusambaratika kwa Mamlaka ya Wapalestina.

Kiongozi wa Israel aliwasili Paris hapo Jumanne akitokea Washington Marekani ambapo alikuwa na mazungumzo mazito na Rais Barack Obama wa Marekani ambaye ametaka kusitishwa kwa ujenzi wa makaazi ya walowezi wa Kiyahudi katika ardhi ya Wapalestina.

Mwandishi: Mohamed Dahman/AFP

Mhariri:Abdul-Rahman