| 21.11.2009 | 04:00 UTC
Westerwelle akutana na Medvedev na Lavrov
MOSCOW
Waziri wa Mambo ya Nchi za Nje wa Ujerumani Guido Westerwelle amesema viongozi wapya waliochaguliwa kuuongoza Umoja wa Ulaya ni watu wenye uwezo na sasa wanakabiliwa na changamoto kubwa.
Kauli hiyo ameitoa mjini Moscow alipokutana na waziri mwenzake wa Urusi, Sergei Lavrov na Rais Dmitry Medvedev, katika ziara yake ya kwanza ya kikazi nchini Urusi. Akizungumza na waandishi habari, Westerwelle alisisitiza nia ya Ujerumani kuendeleza uhusiano mzuri uliopo baina yake na Urusi.
Naye Waziri Lavrov aliutaka Umoja wa Ulaya kuzungumza kwa sauti moja katika kutatua haraka masuala yanayoigusa dunia nzima. Aidha, viongozi hao walizungumzia pia mpango wa nyuklia wa Iran na suala la Afghanistan. Mwishoni mwa ziara yake ya siku moja, Westerwelle alikutana pia na wanaharakati wa kutetea haki za binaadamu nchini Urusi.







