1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Wito wa Wapalestina kutambuliwa kwa taifa lao huru

30 Desemba 2010

Rais wa Mamlaka ya Wapalestina,Mahmoud Abbas leo ataweka jiwe la msingi la ubalozi wa Wapalestina katika mji mkuu wa Brazil, Brasilia.Jumamosi atahudhuria sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Brazil Dilma Rousseff.

https://p.dw.com/p/QlJH
Palestinian President Mahmoud Abbas gestures during a news conference with the German Chancellor Angela Merkel (not in the picture) in the Chancellery in Berlin, Germany, Monday, Feb. 1, 2010. (AP Photo/Gero Breloer)
Rais wa Wapalestina, Mahmoud Abbas.Picha: AP

Mapema mwezi huu Brazil, iliitambua Palestina kama taifa huru kwa kuzingatia mipaka yake iliyokuwepo kabla ya vita vya mwaka 1967.Mkuu wa ujumbe maalum wa Mamlaka ya Wapalestina nchini Brazil,Ibrahim Al Zeben amesema Rais Abbas anataka kukutana na Rais wa Brazil Lula da Silva anaeondoka madarakani, kumshukuru kwa kutambua taifa la Wapalestina.

Palestinian President Mahmoud Abbas (R) talks with his top aide, Saeb Erekat (L), during a press conference following his meeting with Egyptian President Hosni Mubarak (unseen) in Cairo, Egypt on 28 December 2008. Talks focused on the Israeli attacks against Hamas-ruled Gaza, where over 270 people were killed and more than 900 wounded. EPA/KHALED EL-FIQI +++(c) dpa - Report+++
Mpatanishi mkuu Saeb Erekat (shoto) na Rais Abbas wa Wapalestina.Picha: picture alliance/dpa

Kwa upande mwingine,mpatanishi mkuu wa Wapalestina, Saeb Erekat hiyo jana alipozungumza na shirika la habari la Ujerumani DPA, alikanusha ripoti zilizochapishwa katika vyombo vya habari vya Wapalestina na Israel kuwa mwezi wa Januari, atawasilisha katika Baraza la Usalama, pendekezo la kutaka kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina. Amesema, Wapalestina watawasilisha pendekezo la azimio katika Baraza la usalama, lakini, ni kutoa mwito wa kusitisha ujenzi wa makaazi mapya ya Wayahudi kwenye Ukingo wa Magharibi.

Majadiliano ya uso kwa uso kati ya Wapalestina na Waisrael yalivunjika mapema mwezi wa Oktoba baada ya kuanzishwa upya na Marekani mwezi mmoja kabla. Yalivunjika kwa sababu ya Israel kukataa kusitisha kabisa ujenzi wa makaazi mapya katika maeneo ya Wapalestina.Mara kwa mara Wapalestina wameonya kuwa watatumia njia zingine za kidiplomasia badala ya mazungumzo ya uso kwa uso, ili kutimiza lengo lao la kuwa na taifa huru, ikiwa Israel haitokubali sharti la kusitisha kabisa ujenzi wa makaazi hayo.

Miongoni mwa hatua zitakazoweza kuzingatiwa mwakani ni kuomba kutambuliwa kama taifa huru na Umoja wa Mataifa na nchi zingine, kwa kuzingatiwa mipaka iliyokuwepo kabla ya uvamizi wa Israel katika mwaka 1967. Lakini haijulikani lini Wapalestina wanatazamia kuchukua hatua hiyo. Matamshi ya Erekat humaanisha kuwa haitokuwa mapema mwezi Januari mwakani.

Hata hivyo,mpatanishi mwingine wa Kipalestina Nabil Shaath amesema kuwa ukingoni mwa sherehe za kuapishwa kwa rais mpya wa Brazil Januari mosi, Rais Abbas atakuwa na mazungumzo pamoja na baadhi ya marais na mawaziri wakuu wa nchi za Ulaya na Amerika ya Kusini kutaka kuungwa mkono kuhusu kutambuliwa kwa taifa huru la Palestina katika Baraza la Usalama la Umoja wa Mataifa. Brazil, Argentina na Bolivia tayari zimetambua taifa huru la Palestina lenye mipaka ya mwaka 1967.

Mwandishi:P.Martin/DPAE

Mpitiaji:Charo,Josephat