1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za amani ya Mashariki ya kati zakumbwa na misuko suko baada ya Israel kutorefusha muda wa marufuku wa ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi

Oumilkher Hamidou30 Septemba 2010

Walimwengu wameingia mbioni kuyanusuru mazaungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina baada ya kiongozi wa utawala wa ndani wa palastina kutishia kususia mazungumzo hayo

https://p.dw.com/p/PQZ0
Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu(kulia) na mjumbe maalum wa Marekani George MitchellPicha: AP

Juhudi za kimataifa zimeshika kasi kuyanusuru mazungumzo ya amani kati ya Israel na Palastina.Rais Mahmoud Abbas ameonya wapalastina watajitoa katika duru hiyo mpya iliyoanza September pili iliyopita baada ya Israel kutorefusha muda wa kusitisha ujenzi wa makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi katika ardhi za waarabu .

Mjumbe maalum wa rais Barack Obama wa Marekani,George Mitchell yuko tayari ziarani katika eneo hilo,na mwakilishi mkuu wa siasa ya nje ya umoja wa Ulaya bibi Cathrine Ashton amewasili hii leo.Akizungumza na shirika la habari la Reuters mjini Washington jana kabla ya kuelekea Mashariki ya kati, bibi Catherine Ashton amesema changamoto inayoikabili jumuia ya kimataifa ni kumtanabahisha Mahmoud Abbas asalie mazungumzoni.

Rais wa utawala wa ndani wa Palastina,aliyetishia kujitoa mazungumzoni ikiwa Israel haitarefusha muda wa marufuku ya ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi,amesema hatopitisha uamuzi kabla ya kuonana na jumuia ya nchi za kiarabu na kamati kuu ya chama cha ukombozi wa Palastina.

Muakilishi mkuu wa siasa ya nje ya Umoja wa Ulaya amepanga kuzungumza na mjumbe maalum wa rais Barack Obama,katika eneo la mashariki ya kati George Mitchell hii leo,kabla ya kukutana na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahau na baadae na kiongozi wa utawala wa ndani wa Palastina Mahmoud Abbas.

Mjumbe maalum wa rais Barack Obama,George Mitchell alikua na mazungumzo na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahau jana,lakini taarifa yao haijatoa ishara yoyote inayoweza kuepusha mazungumzo kati ya Israel na Palastina yasivunjike. Baadae hii leo George Mitchell amepangiwa kuonana na rais Mahmoud Abbas mjini Ramallah.

Benjamin Netanyahu ambae serikali yake ya muungano inadhibitiwa na vyama vinavyounga mkono ujenzi wa makaazi mepya ya wahamiaji wa kiyahudi,hajajibu miito ya rais Obama na viongozi wengine wa dunia wanaomsihi arefushe marufuku ya ujenzi wa makaazi hayo.

Makaazi ya walowezi ndio sababu ya ghadhabu za wapalastina-Intifadha anasema msemaji wa chama cha ukombozi wa Palastina Fatah Ahmed Assaf:

"Sababu pekee ya Intifadha na upinzani wa wapalastina ni kukaliwa ardhi za wapalastina na Israel.Hivi sasa tunajikuta katika hali ambayo ulimwengu umefika umbali wa kuyaelewa madai ya wapalastina baada ya kuona hadaa ya Israel kwa miongo kadhaa iliyopita.Sisi ni umma unaopigania haki yake ya kuishi,lengo letu ni moja tuu---uhuru."

No Flash Angela Merkel mit dem Emir von Katar Scheich Hamad bin Khalifa Al Thani
Kansela Angela Merkel (kati) na mfalme wa Qatar Sheikh Hamad bin Khalifa Al ThaniPicha: dapd

Qatar na Ujerumani pia zimewatolea mwito waisrael na wapalastina waendelee na mazungumzo ya amani.Mfalme wa Qatar,,Hamad bin Khalifa al Thani ameitolea mwito Israel, baada ya mazungumzo pamoja na kansela Angela Merkel mjini Berlin jana itumie busara na kurahisisha kuundwa dola la Palastina-jambo ambalo anasema amiri huyo "ni kwa manufaa ya usalama wake na utulivu wa eneo hilo".

Kansela Angela Merkel amesema "ni kwa manufaa ya pande zote" ikiwa mazungumzo kati ya Israel na Palastina yataendelezwa.

Mwandishi: Hamidou, Oumilkher/AFP/Reuters

Mpitiaji: Josephat Charo