1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Rais Mahmoud Abbas atishia kutoendelea na mazungumzo ya ana kwa ana na Israel.

29 Julai 2010

Rais Obama aihakikishia Palestina kuwa taifa huru,iwapo watakubali kurejea katika mazungumzo.

https://p.dw.com/p/OXLm
Rais wa Marekani Barack Obama alipokutana na Rais wa mamlaka ya ndani ya wapalestina,Mahmoud Abbas,Juni 9, 2010, Ikulu ya Marekani. Obama ameihakikishia Palestina kutambuliwa kama taifa huru,iwapo itakubali kurejea mazungumzo ya ana kwa na na Israel.Picha: AP

Wakati Mawaziri wa mambo ya nchi za kigeni wa Jumuiya ya Kiarabu wanakutana leo mjini Cairo Misri,Rais wa mamlaka ya ndani ya Wapalestina Mahmoud Abbas amewasili jijini humo kuhudhuria mkutano wa kamati ya Jumuiya hiyo,ambayo inashughulikia mazungumzo baina ya Palestina na Israel,huku suala la kupatikana kwa amani hiyo likiwa bado ni kitendawili.

Maafisa wa Palestina,wameeleza kuwa Rais Abbas anahudhuria kikao hicho,kwa nia ya kuifahamisha Jumuiya ya kiarabu,juu ya vikwazo vinavyokwamisha mazungumzo ya ana kwa ana.

Kamati ya Jumuiya ya nchi za kiarabu inayowahusisha wanadiplomasia muhimu ndani ya umoja huo,inaunga mkono mkakati wa Marekani, wa kuzikutanisha pande hizo kwa mazungumzo ya ana kwa ana,lakini imeeleza kuwa iwapo itashindwa kuzishawishi Israel na Palestina,italirejesha suala hilo kwa baraza la usalama la Umoja wa mataifa.

Israel na Palestina,zinatarajiwa kukutana katika mazungumzo ya ana kwa ana Septemba 1,mwaka huu.

Rais Mahmoud Abbas alikubali kurejea upya katika mazungumzo na Israel kwa masharti kuwa, Israel iwahakikishie Wapalestina kuwa nchi huru,kwa kuzingatia mipaka iliyotengwa mwaka 1967 kati ya wayahudi na Jerusalem pamoja na ukingo wa magharibi wa mto Jordan.

Afisa wa jumuiya ya kiarabu Hisham Yussef, anayeongoza ofisi ya Katibu Mtendaji wa Jumuiya hiyo Amri Moussa,ameliambia shirika la habari la AFP kuwa, suala linalopiganiwa na umoja huo, si kutetea kile ambacho Marekani inakipigania,bali suala la msingi ni kile ambacho wapalestina wanakihitaji kutokana na mtazamo wao.

Kwa upande wake,Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amesema kuwa yupo tayari kukutana na Rais Abbas kuzungumzia mgogoro huo wa kihistoria, baina ya pande hizo mbili,huku akiishutumu Palestina kwa kukataa kurejea katika mazungumzo ya ana kwa ana.

Mpatanishi mkuu wa mgogoro huo,Saeb Erakat,naye ameeleza kuwa Rais wa Marekani Barack Obama,amewahakikishia wapalestina kuwa atahakikisha kuwa Palestina inatambuliwa kama taifa huru,lakini akiweka sharti kwa Palestina kukubali kurejea upya katika mazungumzo na Israel.

Rais Abbas alikataa kuendelea na mazungumzo ya ana kwa ana na Israel,baada ya taifa hilo kuanzisha mashambulizi dhidi ya kundi la Hamas mwaka 2008 katika ukanda wa Gaza,ikiwa ni kujibu shambulio la makombora lililofanywa na kundi hilo.

Lakini Rais Abbas amekuwa akishinikiza mazungumzo mapya baina ya pande hizo,kuendeleza yale yaliyoanza baina yake na Waziri mkuu aliyetangulia wa Israel,Ehud Olmert sharti ambalo Waziri wa sasa Netanyahu,amelikataa.

Wakati huo huo,shinikizo jipya kutoka jumuiya ya kimataifa kutaka mazungumzo mapya kuanza,limetolewa na Waziri wa mambo ya kigeni wa Uhispania,Miguel Angel Moratinos.

Waziri Moratinos katika mazungumzo yake na Waziri wa mambo ya nje wa Israel,Avigdor Lieberman,amemueleza kuwa licha ya kuwepo uzito wa kumalizwa kwa mzozo huo wa kihistoria,lakini amemfahamisha kuwa kama anahitaji amani,ni lazima Israel ikubali mazungumzo ya ana kwa ana.

Rais Abbas na Wazri Netanyahu,pia wamekuwa wakipokea simu za mara kwa mara kutoka kwa viongozi wa umoja wa Ulaya,wakishinikiza juu ya kuhakikisha kuwa mazungumzo hayo,yanafanikiwa kuleta amani.

Hata hivyo,kiongozi wa ngazi ya juu ya kundi la Hamas,Salah al- Bardawil, amemuonya Rais Abbas kuwa asikubali kurejea katika mazungumzo ya ana kwa ana,yatakayosimamiwa na Jumuiya ya kiarabu au Marekani,kwa kueleza kuwa linaweza kusababisha mgawanyiko mkubwa kwa Mamlaka ya wapalestina.

Al- Bardawil amesema kuwa mazungumzo mapya na wale aliowaita kuwa ni maadui zao,litadhidhirisha kuwa Chama cha Fatah kinachoongozwa na Rais Abbas,kitakuwa kimefanya kosa kubwa kwa kurejea katika mazungumzo ambayo yameshindikana kwa zaidi ya miaka 20.

Mwandishi; Ramadhan Tuwa/AFPE/ DPAE

Mhariri;Josephat Charo