1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Operesheni ya kijeshi yaendelea kusini mwa Afghanistan

Prema Martin18 Februari 2010

Pakistan yahofia mikururo ya wakimbizi kufuatia opereshini hiyo ya vikosi vya Isaf na vile vya Afghanistan

https://p.dw.com/p/M53q
Vikosi vya Nato vyawaandama watalibanPicha: AP
Operesheni ya kijeshi inayofanywa na vikosi vya Marekani na Afghanistan dhidi ya Wataliban, inaendelea kwa siku ya sita kusini ya Afghanistan chini ya uongozi wa majeshi ya Marekani. Lakini maafisa wa kijeshi wanasema kuwa operesheni hiyo ya pamoja inakwama kwa sababu ya mabomu yaliyotegwa chini ya ardhi na pia Wataliban kutumia raia kama ngao. Operesheni hiyo dhidi ya ngome ya Wataliban katika eneo la Marjah inatazamwa kwa makini kama mtihani mkuu wa kwanza wa mkakati wa Rais wa Marekani Barack Obama. Lengo ni kumaliza vita vya miaka minane nchini Afghanistan na kuwatimua wanamgambo wenye siasa kali na kuirejesha serikali katika eneo hilo. Mapema juma hili jemadari wa vikosi vya Afghanistan alisema, takriban eneo zima la Marjah na Nad Ali tayari limedhibitiwa. Lakini maafisa rkutoka maeneo ya mapigano wanasema wapiganaji wa Taliban wanajificha nyuma ya raia wa kawaida na wanatega mabomu barabarani na katika majengo. Kwa mujibu wa Jemadari Mohaidin Ghori anaeongoza kiasi ya wanajeshi 4,400 wa Afghanistan katika operesheni hiyo ya pamoja, Wataliban wamewazuia raia kama mateka. Amesema wanawake na watoto wanatumiwa kama ngao.Lakini msemaji wa Taliban amekanusha kutumia binadamu kama ngao. Operesheni hiyo ikiendelea kati kati ya eneo linalolima bangi katika Wilaya ya Helmand, maelfu ya watu wamekimbilia mji wa Lashkar Gah na mikoa mingine ya jirani na eneo la Nimroz ambako Shirika la Umoja wa Mataifa WFP linaloshughulikia mipango ya chakula duniani, limegawa chakula kwa mamia ya familia zilizokuwa na njaa. Kiasi ya watu 80,000 wanaishi katika eneo hilo. Lakini kwa mujibu wa Amnesty International linalotetea haki za binadamu duniani, kama raia 10,000 wamelikimbia eneo hilo.Shirika hilo limeonya kuwa maelfu wengine wamenasa katika maeneo ya mapigano.
Yousuf Raza Gilani und Richard Holbrooke
Waziri mkuu Raza Gilani wa Pakistan na mjumbe maalum wa Marekani Richard HolbrookePicha: AP
Wakati huo huo,hii leo nchi jirani Pakistan imeelezea wasiwasi kuhusu uwezekano wa wakimbizi wa Kiafghanistan na wanamgambo kuvuka mpaka kama ilivyotokea mwaka 2001 kufuatia uvamizi wa Afghanistan na hivyo kusababisha harakati za wanamgambo katika eneo la mpakani. Waziri Mkuu wa Pakistan Yousuf Raza Gilani aligusia suala hilo alipokutana na Richard Holbrooke alie mjumbe maalum wa Marekani katika Afghanistan na Pakistan. Amesema ni matumaini yake kuwa majeshi ya Marekani na vikosi vya kimataifa ISAF vitazingatia wasiwasi wa Pakistan kuhusu wakimbizi na wanamgambo kutoka kusini mwa Afghanistan. Mwandishi: Martin,P/AFPE/RTRE Mhariri: Hamidou,Oummilkheir