1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Iran na dimba la Ujerumani magazetini

Oumilkher Hamidou8 Februari 2010

Rais wa Iran achezea moto wasema wahariri wa Ujerumani

https://p.dw.com/p/LvWq
Katibu mkuu wa jumuia ya kujihami ya NATO Anders Fogh Rasmussen (kulia) na waziri wa ulinzi wa serikali kuu ya UjerumaniPicha: picture alliance / dpa

Mkutano wa usalama mjini Munich, na kinyang'anyiro cha madaraka katika shirika la kabumbu nchini Ujerumani DFB ni miongoni mwa mada zilizochamabuliwa na wahariri wa magazeti ya Ujerumani hii leo.

Tuanzie lakini Munich ambako wahariri wanahisi Iran imelitumia jukwaa la mkutano wa usalama wa kimataifa ili kuicheza shere jumuia ya kimataifa.Gazeti la " NORDWEST-ZEITUNG la mjini Oldenburg" linaandika:

"Lilikua pigo jengine hilo.Vuta nikuvute kuhusu mradi wa kinuklea wa Iran inaingia katika awamu nyengine.Hata kama watu walikua tayari kuziamini ahadi za utawala wa mjini Teheran za kushirikiana na jumuia ya kimataifa,utayarifu huo hivi sasa umechujuka kutokana na hotuba ya waziri wa mambo ya nchi za nje wa Iran katika mkutano wa usalama mjini Munich.Iran haijaachana na mipango yake ya kutaka kujitengenezea silaha za kinuklea.Kwa mara nyengine tena mvutano umezidi makali.Wakati umewadia sasa,sio kuzungumzia juu ya shambulio la kijeshi,bali hasa kusaka uungaji mkono wa walio wengi ili kuiwekea vikwazo zaidi serikali ya mjini Teheran.Jumuia ya kimataifa na jumuia ya kujihami ya Magharibi NATO zinajikuta njia panda hivi sasa.

Gazeti la NORDBAYERISCHER KURIER la mjini Bayreuth linahisi rais Ahmedinedjad anacheza na moto.Gazeti linaendelea kuandika:

Rais wa Iran anacheza mchezo mbaya sana:Kwanza anazusha matumaini na muda si muda anayamwagia mchanga.Anamtuma waziri wake wa mambo ya nchi za nje katika mkutano wa usalama mjini Munchen ili kuleta mfarakano ndani ya jumuia ya kujihami ya magharibi.Mara senetor wa Marekani Joe Liebermann akaishiwa na subira na kutishia Teheran itahujumiwa kijeshi.Ahmadinedjad anatanga tanga kwasababu nchini mwake kunatokota.Wananchi wa Iran na hasa wale ambao hawaungi mkono msimamo wa mayatollah,hawataki kufuata mkondo wa vita ,wakihofia usije ukawaangamiza.Ishara za kupalilia mivutano zimechomoza mwishoni mwa wiki.Wananchi wa Iran hawajui wafanye nini,wanataraji tuu kwamba wenye usemi wataepukana na balaa la mgogoro wa kijeshi.

Mada yetu ya pili magazetini inahusu mvutano ndani ya shirikisho la kabumbu la Ujerumani DFB.Gazeti la Stuttgarter Zeitung linaandika:

Deutschland Fußball Präsident Theo Zwanziger
Mwenyekiti wa shirikisho la kambumbu la Ujerumani Theo ZwanzigerPicha: picture alliance / dpa

Kilichohanikiza magazetini mnamo siku za hivi karibuni,kuhusiana na madai ya kurefushwa mkataba wa kocha wa timu ya taifa Joachim Löw na meneja wa timu ya taifa ya kabumbu Oliver Bierhoff,kinabainisha ukosefu wa kutambua hali namna ilivyo,upotofu na kiu ya madaraka na mali.Pekee fedheha iliyosababishwa na pande zote mbili, ni sababu ya kutosha,kuwafukuza wote wahusika.Hata wakati wa enzi za mwenyekiti wa zamani wa shirikisho la kambumbu la Ujerumani DFB,Gerhard Mayer-Vorfelder ,habari za kuudhi zilikua zikivuja toka makao makuu ya soka la Ujerumani mjini Frankfurt-lakini katika enzi za sasa za aliyeshika nafasi yake Theo Zwanziger,jungu la njama na fitna laonyesha kuzidi kutokota.

Mwandishi:Hamidou,Oummilkheir /Dt Presse

Mhariri:Abdul-Rahman