1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Juhudi za kufufua utaratibu wa amani ya Mashariki ya kati

Oumilkher Hamidou29 Desemba 2009

Waziri mkuu wa Israel ziarani mjini Cairo kwa mazungumzo pamoja na rais Hosni Mubarak wa Misri

https://p.dw.com/p/LGTM
Waziri mkuu wa Israel Netanyahu akizungumza na rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu amewasili Misri leo mchana kwa mazungumzo pamoja na rais Hosni Mubarak .Utaratibu wa amani kati ya Israel na Palastina ndio kiini cha mazungumzo hayo.

Mazungumzo kati ya rais Hosni Mubarak na waziri mkuu wa Israel Benjamin Netanyahu yamemalizika bila ya viongozi hao wawili kusema kitu.Hata hivyo ofisi ya waziri mkuu Netanyahu ilisema baadae" mazungumzo hayo yalikua ya kina na ya dhati."

"Wamezungumzia namna ya kuufufua utaratibu wa amani pamoja na wapalastina na juhudi za kurejea nyumbani mwanajeshi wa kiisrael Gilad Shalid anaeshikiliwa na wanamgambo wa Hamas.

Ziara hiyo imefanyika katika wakati ambapo serikrali ya

rais Barack Obama wa Marekani,inajiandaa ,kwa mujibu wa wanadiplomasia wa nchi za kiarabu na za magharibi mjini Cairo,kuwatumia waisrael na wapalastina risala mbili za udhamini kwa lengo la kufufua mazungumzo yaliyokwama tangu Israel ilipoihujumu Gaza mwishoni mwa mwaka 2008.

Kwa mujibu wa wanadiplomasia wa nchi za kiarabu na za magharibi mjini Cairo,Misri inahusika na juhudi za kidiplomasia zenye lengo la kufufua mazungumzo ya amani.

Muda mfupi kabla ya waziri mkuu wa Israel kuwasili mjini Cairo,waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri,Ahmed Aboul Gheit alikosoa vikali mpango wa serikali ya Israel wa kuruhusu ujenzi wa makaazi mia kadhaa ya wayahudi katika eneo la mashariki la mji wa Jerusalem.

"Ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi unavuruga juhudi za kufufua mazungumzo yaliyolenga kuundwa dola la Palastina" amesema waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri-Ahmed Aboul Gheit akinukuliwa na shirika la habari la Misri-MENA.

"Tabia kama hiyo inawafanya watu wajiulize kama kweli Israel inataka papatikane ufumbuzi wa kudumu wa mzozo pamoja na wapalastina na unawafanya watu waamini kwamba Israel inataka kujitoa na majukumu ya kupatikana amani ya haki na ya kudumu"-mwisho wa kumnukuu waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri.

Der neue Nahost Vermittler der US Regierung George Mitchell in Kairo, Ägypten
Mjumbe maalum wa rais Barack Obama katika eneo la Mashariki ya kati,George MitchellPicha: AP

Tangazo la serikali ya Israel la kuruhusu ujenzi wa makaazi mepya ya wayahudi katika eneo la mashariki la Jerusalem limezusha ghadhabu pia nchini Marekani na katika Umoja wa Ulaya.

Waziri wa mambo ya nchi za nje wa Misri Ahmed Abu Gheit anatazamiwa kufika ziarani mjini Washington mapema mwezi ujao,nae mjumbe maalum wa rais Barack Obama katika eneo la mashariki ya kati,George Mitchell anatarajiwa pia kulitembeleya eneo hilo hivi karibuni.Lengo la ziara hiyo ni kuwakabidhi waisreal na wapalastina waraka wa udhamini ili kuweza kutia njiani mazungumzo ya amani.

Mbunge wa zamani wa mrengo wa shoto kutoka Israel,Yossi Beilin ameliambia shirika la habari la Reuters kwamba Netanyahu anakurubia kufikia makubaliano pamoja na utwala wa Marekani kuhusu utaratibu wa kufufua mazungumzo ya amani.

Hoja hizo zimesutwa hata hivyo na msemaji wa waziri mkuu Netanyahu,Mark Regev,aliyesema bwana Yossi Beilin anazungumza kwa niaba yake mwenyewe.

Mwandishi Hamidou Oummilkhheir (AFP,Reuters)

Mhariri:Yusuf Saumu Ramadhan