1. Nenda kwenye maudhui
  2. Nenda kwenye orodha kuu
  3. Nenda tovuti zaidi za DW

Hosni Mubarak akaimu madaraka

11 Februari 2011

Nchini Misri ,Rais Hosni Mubarak amelihutubia taifa na akayakaimu majukumu ya uongozi kwa makamu wake Omar Suleiman kinyume na ilivyotarajiwa na maelfu ya waandamanaji.

https://p.dw.com/p/10FUa
Rais Hosni Mubarak wa MisriPicha: AP

Wanaharakati hao wamekuwa wakikutana katika uwanja wa Tahrir kwa siku ya 18 sasa kwa minajili ya kumshinikiza Rais Hosni Mubarak ajiuzulu.Itakumbukwa kuwa kiongozi huyo amekuwa madarakani kwa kipindi cha miaka 30.

Waandamanaji hao wa Misri wameahidi kuendelea na harakati zao mjini Cairo hii leo ili kumuongezea mbinyo Rais Hosni Mubarak na naibu wake wajiuzulu.Wengi wao walikusanyika kwenye uwanja wa Tahrir jana usiku wakiisubiri hotuba ya Rais Hosni Mubarak ya kujiuzulu, ila badala yake alimkabidhi Makamu wa rais,Omar Suleiman,madaraka jambo lililowaghadhabisha.

Flash Galerie Kabinettssitzung in Kairo
Rais Hosni Mubarak kikaoni na makamu wa rais Omar SuleimanPicha: picture alliance / dpa

Mwezi wa Septemba

Rais Hosni Mubarak alieleza kuwa ataendelea kuwa uongozini mpaka mwezi wa Septemba na akaahidi kuwa bora afe nchini mwake Misri badala ya kuenda uhamishoni kokote kule.Pindi baada ya hotuba ya Rais Mubarak,Makamu wa Rais Omar Suleiman aliwaomba waandamaanaji hao warejee makwao,kauli zilizoitikiwa na vitisho vya kulivamia kasri la kiongozi huyo.


Jeshi ndiye muokozi? 

Katika ujumbe wake kwenye mtandao wa kijamii wa Twitter,mwanasiasa wa upinzani Mohammed Elbaradei aliyekuwa pia kiongozi wa zamani wa Shirika la Atomiki la Umoja wa Mataifa IAEA,alieleza kuwa Misri iko hatarini na akalitolea wito jeshi la nchi hiyo kuwaokoa wananchi.

Wengi ya waandamanaji hao waliokusanyika kwenye uwanja wa Tahrir wanataka kufanya mgomo mkubwa zaidi hii leo kadhalika jeshi kuamua mkondo watakaoufuata.Taarifa zinaeleza kuwa maafisa wa kijeshi wameuzingira uwanja huo wa Tahrir. 

Flash-Galerie Proteste in Kairo am 02.02.2011
Waandamanaji wakiwa uwanja wa Tahrir:maandamano makubwa kufanyika Ijumaa 11.02.2011Picha: dapd

Wakati huohuo,balozi wa Misri nchini Marekani,Sameh Shoukry, aliyehojiwa na shiria la habari la CNN; alisisitiza kuwa makamu wa rais,Omar Suleiman, ndiye kiongozi mteule na msimamizi mkuu wa jeshi la nchi hiyo.

Kwa upande mwengine,hali hiyo ya kisiasa ya Misri, imewawia vigumu viongozi wa mataifa ya magharibi,hususan Marekani.Umoja wa Ulaya umemueleza Rais Hosni Mubarak kuwa muda wake wa kuondoka umewadia nayo Ujerumani imesisistiza kuwa hotuba yake hiyo kamwe haijaituliza jamii ya kimataifa.

Kikao cha dharura

Duru zinaeleza kuwa,muda mfupi baada ya hotuba hiyo,rais wa Marekani Barack Obama alifanya kikao cha dharura na kundi lake la wataalam wa usalama wa kitaifa.Hata hivyo matokeo ya mkutano huo bado hayajabainika.Uingereza kwa upande wake imesema kuwa inayatathmini matukio yote ya Misri na jambo la msingi ni kuyapa umuhimu matakwa ya raia wa Misri.

Mtazamo huo unaungwa mkono na Waziri Mkuu wa Australia Julia Gillard anayesisitiza kuwa kuna umuhimu wa kudumisha amani katika kipindi hicho kigumu.

Kwa upande wake,Ufaransa imekiri kuwa hatua ya aliyoichukua Rais Hosni Mubarak ni sahihi.Rais Nicolas Sarkozy wa Ufaransa alisisitiza kuwa hatua hiyo kamwe haiepukiki na ndiyo iliyo sahihi.

Mkuu wa sera za Umoja wa Ulaya,Catherine Ashton bado anashikilia kuwa kuna umuhimu mkubwa wa yeye kuizuru Misri haraka iwezekanavyo ijapokuwa uongozi wa nchi hiyo una pingamizi

Kwa upande wake,Israel imeusisitizia umuhimu wa kuipa Misri muda ili kuwazuwia walio na misimamo mkali kupata mwanya wa kuingia madarakani.Kauli hizo zimetolewa na Waziri wa Ulinzi wa Israel,Ehud Barak, aliyezungumza na kituo cha televisheni cha Marekani cha ABC. 

Entwicklung der Unruhen in Ägypten Flash-Galerie
Kiongozi wa IAEA wa zamani Mohamed El Baradei:Jee ndiye muokozi wa Wamisri?

Mkataba wa amani na Israel

Akizungumza na waandishi wa habari baada ya kikao chake na katibu MKuu wa Umoja wa Mataifa Ban Ki Moon,Waziri wa Ulinzi wa Israel Ehud Barak alisema kuwa hatma ya Wamisri iko mikononi mwao.Hata hivyo kulingana na kiongozi huyo,bado kuna matumaini katika hali hiyo ngumu ya kisiasa ya Misri.

Misri iliyofikia mwafaka wa kudumisha amani na Israel mwaka 1979,iliubadili mkondo wa siasa za eneo la Mashariki ya kati.Ifahamike kuwa Misri ni nchi ya kwanza ya kiarabu kuchukua hatua hiyo.Hofu iliyopo ni kuwa,baadhi ya wanasiasa wa Israel na wa mataifa ya magharibi wanahisi kuwa makubaliano hayo ya amani huenda yakavurugika iwapo majukumu ya kuiongoza Misri yataangukia mikononi mwa wanasiasa walio na msimamo mkali. Mwandishi:Mwadzaya,Thelma-RTRE/AFPE